NA TIMA SALEHE, DAR ES SALAAM
MAHAKAMA ya usuluhishi wa michezo (CAS) inaanza kushuhulikia rufaa ya klabu ya Yanga dhidi ya mchezaji wa klabu ya Simba Bernard Morrison leo.
Taarifa hiyo iliyotolewa jana na uongozi wa Yanga kupitia mtandao wao wa kijamii wa Instagram.
Uongozi wa Yanga umeeleza kwamba inapenda kuwataarifu mashabiki na wanachama wao juu ya maendeleo ya kesi yao dhidi ya Bernard Morrison ambayo inaendelea kwenye mahakama ya usuluhishi wa michezo (CAS).
Kwa mujibu wa sheria na taratibu za uendeshaji wa mashauri katika mahakama hiyo, hairuhusiwi kueleza mwenendo wa kesi mpaka itakapotolewa maamuzi.
Hata hivyo Yanga inapenda kuwajuza kuwa kilichochelewesha kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo ni pingamizi la awali la (Preriminary Objection) la mamlaka ya CAS kusikiliza rufaa hiyo lililowekwa na mjibu rufani Bernard Morrison likitaka kesi hiyo irudishwe nchini.
Baada ya ya Mahakama kusikiliza hoja za pande zote mbili juu ya pingamizi hilo , CAS imelitupilia mbali pingamizi hilo la Morrison hivyo itaanza kusikiliza rasmi kesi ya msingi Juni 2.