SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imewasilisha bajeti yake katika Baraza la Wawakilishi, tukitegemea sasa wajumbe hao wanaowawakilisha wananchi wote wa Zanzibar wataucheza vizuri mpira uliopo uwanjani kwao.

Kwa ujumla serikali inaomba Baraza la Wawakilishi liidhinishe makadirio ya mapato ya serikali kwa kukusanya shilingi trilioni 1,829.9 kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Kati ya fedha hizo shilingi bilioni 947.1 zitatumika kwa ajili ya utekelezaji wa kazi za kawaida za serikali na shilingi bilioni 882.8 kwa ajili ya utekelezaji wa mpango wa maendeleo.

Tunaelewa kuwa hii ni bajeti ya kwanza ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya awamu ya nane, hata hivyo utekelezaji wake hutatofautiana sana na vipaumbele vya awamu zilizopita.

Kwa mfano bajeti hii inakwenda kutekeleza mpango na mikakati ya maendeleo wa Zanzibar ikiwemo MKUZA III pia bajeti inakwenda kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Tunaelewa kuwa kuzipata shilingi trilioni 1,829.9 ni kazi kubwa, lakini tunaamini itakuwa rahisi sana fedha hizo kupatikana endapo kila Mzanzibari kwa nafasi yake atatekeleza wajibu wake.

Wakati mpira huo kwa wakati huu ukiwa mezani kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, wananchi wanategemea mijadala ya viongozi hao itakuwa na afya katika kufanikisha bajeti hiyo iliyobeba mustakbali wa maisha ya wananchi.

Tunategemea sana wajumbe wa baraza letu la wawakilishi wataionesha serikali maeneo ambayo yataibua vyanzo vipya vya mapato vitakavyokuwa vya uhakika na endelevu ambavyo vitafanikisha kupatikana kwa shilingi trilioni 1,829.9 au hata zaidi hapo.

Serikali kwa upande wake inapaswa kuonesha ukali usio na huruma dhidi ya wale wanaovujisha mapato kwa manufaa yao binafasi kwenye taasisi mbalimbali za umma.

Kwa ushauri wetu katika kutekeleza hilo, serikali inapaswa kutafuta tochi yenye mwanga mkali kuviangalia vitengo vya manunuzi katika taasisi za umma kwani huko kuna uhujumu mkubwa wa fedha za umma.

Tochi ya serikali pia izimurike taasisi na mamlaka zinazokusanya fedha kwa sababu zipo baadhi yao zimekosa imani kwa walipa kodi wakiamini fedha wanazokusanya hazifiki kunakostahiki.

Tunayazungumza haya kwa sababu bado fedha za umma zinapigwa sana kiasi kwamba hata repoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali inaonesha hali hiyo.

Yapo mengi sana kwenye taasisi za umma ikiwemo matumizi ya ovyo, safari zisio na tija kwa taasisi, taasisi nyengine kutopeleka makusanyo katika mfumo wa hazina kwa kisingizio cha kupata hasara na mengineyo.

Sisi hatuna wasiwasi na ukusanyaji wa fedha hizo za bajeti, lakini kama tutakuwa na msimamo thabiti na kuwa makini kwa kila eneo kusimamiwa kama inavyotahiki.

Hata hivyo, tukiachilia kila mtu afanye anavyotaka kama yalivyo mazoea yetu, bajeti hiyo itakuwa ya tarakimu itakayobakiwa katika vitabu.