ULIMWENGU unaadhimisha siku ya mapambano dhidi ya matumizi ya dawa kulevya, ambapo kwa Zanzibar kama zilivyo nchi nyengine masikini, matumizi ya uraibu huo umesababisha janga la kiuchumi, kiafya na mmong’onyoko wa maadili.
Dawa za kulevya ni kemikali ambapo zinapongia katika mwili wa binaadam huathiri ubongo wa mtumiaji na kumsababishia kuwa na matendo, hisia, fikra na muonekano tofauti na mtazamo wa jamii.
Tunaposema dawa za kulevya zimeleta athari kiuchumi tuna maana kwamba walioathirika wengi ni kundi la vijana ambao ndio tegemezi la taifa ama nguvu kazi katika ujenzi wa uchumi.
Dawa za kulevya zinasababisha janga la kiafya kwani vijana wengi wanaotumia dawa hizo huwa na afya dhaifu, lakini takwimu zinabainisha kuwa ndio waathirika wakubwa kwenye maambukizi ya HIV na ugonjwa wa kifua kikuu.
Taarifa zinaeleza kuwa wagonjwa wengi waliolazwa katika hospitali ya wagonjwa wa akili iliyopo Kidongochekundu ni watumiaji wa dawa za kulevya, ambao wameathirika kutokana na matumizi ya dawa hizo.
Mtumiaji wa dawa za kulevya huwa hana soni, kwani anaweza kufanya vitendo vya ajabu vikiwemo vya uchafu mbele za watu, lakini pia huwa na kawaida ya wizi ili apate vijisenti vya kumugharama za kununulia dozi.
Bila shaka hii ni siku muhimu ambayo kama wazanzibari, kama wakuu wa familia kama sehemu ya jamii, kila mmoja atapata nafasi ya kutafakari kwa namna gani tunaweza kulimaliza tatizo hili katika jamii yetu.
Kwa tunavyofahamu vita ama mapambano dhidi ya dawa za kulevya, si jukumu la mamlaka za serikali pakee, bali hili ni suala la jamii nzima kuhakikisha inasimama kwa kuhakikisha linamalizwa na kutokomezwa kabisa.
Sababu kubwa ya kuchukua muda mrefu kwenye mapambano dhidi ya dawa za kulevya inatokana na kwamba sehemu kubwa ya jamii inadhana kuwa mamlaka za serikali ndizo zitakazolimaliza tatizo hilo, wakati sio kweli.
Kwa mujibu wa taarifa Zanzibar inakadiriwa kuwa na watu 10,000 wanaotumia dawa za kulevya, idadi ambayo inaelezwa kuwa imekuwa ikiongezeka hali inayochangia ongezeko la vitendo vya kihalifu.
Ni kweli kabisa mamlaka za serikali zina nafasi yake muhimu, lakini jamii nayo kwa sehemu kubwa nayo inatakiwa itekeleza wajibu mkubwa kwa kushirikiana na mamlaka za serikali kuwafichua wanaoendesha bishara hizo ambazo wanaishi katika jamii.
Dawa za kulevya Zanzibar sio tatizo la kwenye miji tu, bali limetanuka na hivi sasa bishara hiyo imeenea karibu vijiji vyote vya Unguja na Pemba hasa katika maeneo yaliyostawi kwa utalii.
Wakati tukiadhimisha siku hii, tunapaswa kutafakari njia mbalimbali zitakazotusaidia kulimaza tatizo hili, ikiwemo muundo wa mamlaka tume ya dawa za kulevya na sheria zetu kwa kiasi gani zinatusaidia kukabiliana nalo?
Kama kweli tunataka kulimaliza tatizo la dawa za kulevya lazima tuwe na mamlaka nyenye mamlaka kamili ya kupambana dawa za kulevya na sio kuwa na mamlaka yenye majukumu nusu.
Inakuwaje tume ya kuratibu na kudhibiti dawa za kulevya haina nguvu za kuwakamata na kuwashitaki watuhumiwa wanaoshikwa na dawa hizo?
Wakati umefika mamlaka za serikali na jamii kwa pamoja tukae tuutafakari ukubwa wa tatizo la dawa za kulevya na mustakbali wa hatima ya nchi yetu.