SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, imesema ina mpango wa kukikarabati kituo cha afya cha shehia ya Shamiani Mwambe ili kiweze kutoa huduma bora kwa wananchi.

Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii , Wazee, Jinsia na Watoto,Nassor Ahmed Mazrui, aliyasema hayo wakati akimjibu suala la msingi Mwakilishi wa jimbo la Kiwani, Mussa Foum Mussa, alietaka kujua wizara hiyo ina mpango gani wa kukifanyia ukarabati kituo hicho ili kutatua changamoto hizo sambamba na kukitafutia daktari.

Alisema wananchi wengi wa shehia hiyo wanategemea zaidi kupata huduma katika kituo hicho, hivyo serikali itahakikisha inakiimarisha kituo hicho ili kiende sambamba na malengo yaliyokusudiwa.

“Nikweli kituo cha Shamiani Mwambe ni kibovu na kinavuja wakati wa mvua na kama Wizara inalitambua kwa kina suala hili”, alisema.

Alisema kwa kuwa vituo vya afya vilikua kwenye ugatuzi chini ya Tawala za Mikoa na kwasasa vimesharejeshwa katika wizara husika, hivyo ukarabati huo utafanywa kupitia makusanyo ya ndani ya baraza la Mji Mkoani kwa kipindi cha April hadi June 2021.

Aidha, alibainisha kuwa, Baraza hilo limetenga shilingi millioni saba katika kufanya ukarabati huo.

“Ni kweli kituo hicho hakina daktari lakini hata hivyo kutokana na uhaba wa wafanyakazi katika baadhi ya vituo, Wizara tayari imeshawasilisha maombi ya ajira serikali kuu katika kutatua changamoto hii na hospitali nyengine”, alisema.