NA MOHAMMED ALI

UONGOZI wa mkoa Mjini Magharibi umewahakikishia wananchi wa mkoa huo kuwa utashirikiana kwa karibu na sekta mbali mbali ili kuzipatia ufumbuzi kero zinazowakabili katika shehia zao.

Ahadi hiyo imetolewa na Mkuu wa mkoa huo, Idrissa Kitwana Mustafa, katika mkutano wake wa kwanza wa kukutana na wananchi katika shehia kwa ajili ya kusikiliza kero zao uliofanyika katika shehia ya Kijichi, wilaya ya Magharibi ‘A’, Unguja.

Akiambatana na baadhi ya viongozi na watendaji wa sekta mbali mbali, Kitwana aliziagiza taasisi hizo kuyashuhulikia kwa vitendo malalamiko yatakayotolewa wakati wa mikutano yake na wananchi itakayofanyika katika shehia zote za mkoa huo.

Akizungumzia baadhi ya kero na changamoto zilizotolewa na wananchi ikiwemo ya maji na umeme, Kitwana amelitaka Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) na Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA), kuzifuatilia na kuzipatia ufumbuzi kero zinazowakabili wananchi eneo hilo.

“Badala ya kusubiri wananchi walalamike ndipo mfanyie kazi malalamiko hayo ni vyema mkawa na utaratibu wa kuzipatia ufumbuzi changamoto za watu wetu pale mnapopata taarifa,” alieleza Kitwana.

Alisema wananchi wamekuwa wakilipa kodi na ada ya huduma kwa taasisi hizo, hivyo wana wajibu wa kupatiwa huduma bora.

Akijibu malalamiko ya wananchi kuhusu tatizo la kuchelewa kupata huduma za masheha, Mkuu huyo wa mkoa aliwataka Masheha kuacha urasimu katika kuwahudumia wananchi.

“Masheha wana wajibu wa kuwapa huduma wananchi wote bila ya ubaguzi wa aina yoyote ile hivyo sitasita kuwachukulia hatua masheha watakaokuwa wanawasumbua wananchi pale wanapofuata huduma,” alisema Kitwana.

Akizungumza wakati wa mkutano huo, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA), Kazija Mussa Msheba, aliahidi kulipatia ufumbuzi tatizo la maji katika shehia hizo kabla ya mwezi wa Agosti mwaka huu.

Alisema ZAWA imeandaa mpango wa utekelezaji utakaotatua kero za maji katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar kupitia bajeti mpya ya serikali itakayoanza mwezi Julai, mwaka huu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Umeme (ZECO), Msheba Haidar Msheba, alisema kuwa shirika hilo linatarajia kufungua matawi yake katika mikoa yote ya Zanzibar ili kurahisisha upatikanaji huduma kwa wananchi.

Aidha aliwataka wananchi kutosita kufikisha kero zinazowakabili  katika shirika hilo kwa kuwa lipo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.

Awali wananchi wa Shehia za Bububu na Kijichi walilalamika mbele ya Mkuu huyo wa mkoa zikiwemo kero za kukosekana kwa huduma ya maji, barabara za ndani, mitaro ya kupitishia maji ya mvua, wizi na tatizo la ajira.

Mikutano hiyo ya Mkuu wa mkoa kukutana na wananchi na kusikiliza kero zinazowakabili, inatarajiwa kuendelea katika shehia zote za mkoa huo.