NA MWAJUMA JUMA

MABINGWA wapya wa ligi kuu ya Zanzibar msimu wa 2020/2021 KMKM, wanatarajiwa kukabidhiwa zawadi yao kesho Ijumaa ya  Juni 11.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Sheha Mohammed alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi huko ofisini kwake Amaan.

Alisema bingwa huyo atashuka katika dimba la Amaan kucheza na Black Sailor, anatarajiwa kukabidhiwa zawadi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ Masoud Ali Mohammed ambaye atakuwa mgeni rasmi.

“Tunatarajia waziri ndiye atakuwa mgeni rasmi tushapeleka maombi lakini hatujapata majibu,” alisema.

Hata hivyo alisema mpaka sasa bodi yao inafahamu kwamba bingwa huyo atakabidhiwa zawadi ya kikombe pamoja na medali.

Alifahamisha kwamba ligi hiyo haina mfadhili hivyo hawawezi kutoa ahadi nyingine, hasa ikizingatiwa kuwa kanuni inaeleza wazi kuwa bingwa atapewa zawadi ya kombe na kama itatokea zawadi nyengine watapewa.

“Ni kombe tu ndilo atakalopewa bingwa wetu, kama itatokea zawadi nyengine basi tutampatia, ila kanuni yetu inatuelekeza bingwa atapewa kombe na medali”, alisema.

Ligi hiyo ilikuwa ikishirikisha timu 12 kesho inafikia tamati

ambapo mabingwa hao wametwaa ubingwa wakiwa na pointi 41.