NA KHAMISUU ABDALLAH

MKUU wa Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM), Commodore Azana Hassan Msingiri amesema mipango ya kikosi hicho ni kuuza dawa kwa jumla kwa hospitali zote za Zanzibar.

Kauli hiyo aliitoa wakati akizungumza na Mohammed Mbaye kutoka kampuni ya OIL COM ya jijini Dar es Salaam aliyefika Makao Makuu KMKM Kibweni na ujumbe wake kwa lengo la kuwekeza miradi mbali mbali katika kikosi hicho.

Alisema, KMKM ipo katika kujiimarisha zaidi ili kuona inajitegemea wenyewe na kuiongezea mapato serikali kupitia miradi mbalimbali watakayoianzisha ambayo italeta tija kwa jamii na taifa kwa ujumla.

Msingiri alibainisha kuwa akiwa mkuu wa kikosi hizho atahakikisha kinapiga hatua hasa katika uzalishaji mali na kuibua miradi ambayo itakiwezesha kuimarika zaidi.

Aidha alibainisha kuwa tayari wameshafanya mazungumzo na muwekezaji Mo Dewji ili aweze kuwekeza katika hospitali hiyo kutokana na muwekezaji huyo kumiliki kiwanda cha dawa.

Sambamba na hayo alisema lengo la kikosi hicho ni kujenga bohari kubwa kwa ajili ya kuhifadhia dawa hizo.

Kwa upande wake Mohammed Mbaye alisema dhamira yake kwenda katika kikosi hicho ni kuangalia maeneo ya kuwekeza miradi mbali mbali ambayo itafaa kuwekezwa kutokana na eneo husika.

Alisema ni jambo la lazima kuunganisha nguvu pamoja na ujuzi ili kumpa nguvu Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi katika ahadi alizotoa ikiwemo swala la ajira 300,000 alizoahidi kwa vijana wa Unguja na Pemba.

Hata hivyo alisema ameamua kuwekeza KMKM kutokana na kuona ndio sehemu sahihi kwani kikosi hicho kina uwezo, nguvu kazi, heshima na kina maeneo makubwa kwa ajili ya uwekezaji hivyo wanastahiki kusaidiwa.

Aidha muwekezaji huyo alisema amevutiwa zaidi na maeneo waliyooneshwa ya Kibweni  na Maisara ambayo yanafaa kwa uwekezaji.

Naye Kaimu Mkuu wa Utawala KMKM, Kamanda Juma Saleh Seif, aliwapongeza wawekezaji hao kwa kujiamini na kuona kikosi hicho ndio pahali sahihi kwa kuweka uwekezaji wao.

Hata hivyo alibainisha kuwa wawekezaji hao wamekuja wakati muafaka kwani kikosi hicho kimo katika mipango ya kuzalisha na tayari kimeshanunua boti kwa ajili ya uvuvi lakini pia ujenzi wa bekari kwa ajili ya uuzaji wa mikate ambao karibu utakamilika.