NA MWAJUMA JUMA

MAAFANDE wa Kikosi Maaalumu cha Kuzuia Magendo KMKM wametwaa ubingwa wa michuano ya ‘KMKM Day’ kwa kuwafunga KVZ bao 1 – 0 katika mchezo wa fainali uliochezwa usiku wa kuamkia jana.

Mchezo huo ambao ulichezwa katika uwanja wa Amaan ulikuwa na ushindani kiasi huku KMKM wakiwa ndio waandaaji wa michuano hiyo wakijaribu kufanya kila liwezekanalo ili kombe hilo libakie nyumbani kwao.

Katika mchezo huo Mgeni rasmi alikuwa ni Mkuu wa mkoa wa Mjini Magharibi, Idrissa Kitwana Mustafa, alieambatana na Mkuu wa wilaya ya Mjini, Rashid Simai Masaraka pamoja na viongozi wa juu wa KMKM akiwemo commodore Azana Hassan Msingiri.

KMKM ambayo ilishusha kikosi chake kamili katika michuano hiyo ikilinganishwa na KVZ ambao waliwatumia wachezaji wengi wa timu ‘B’ hadi mapumziko walikuwa wakiongoza kwa bao 1 – 0.

Bao hilo la pekee liliwekwa kimiyani na mchezaji wake Salum Akida Shukuru mchezaji ambae awali alikuwa akiichezea timu ya KVZ kubwa.

Bingwa wa michuano hiyo atakabidhiwa kombe na shilingi 500,000 wakati mshindi wa pili atapata kitita cha shilingi 300,000, zawadi ambazo zitakabidhiwa siku ya kilele Julai Mosi mwaka huu.