NA TATU MAKAME

WIZARA ya Utalii na Mambo ya Kale imetoa ruhusa ya uwekezaji na kukodisha majumba ya Mji Mkongwe kwa majengo yote yanayomilikiwa na serikali, watu binafsi, majengo ya wakfu pamoja na yanayomilikiwa na Shirika la nyumba.

Waziri wa Wizara hiyo Lela Muhamed Mussa alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuwa hatua hiyo imelenga kuyaweka katika hali nzuri.

Aidha serikali imetangaza kuwekeza katika miundombinu mbali mbali iliyomo ndani ya maeneo ya uhifadhi Mji Mkongwe ili kuongeza ubora wa mji na kwamba majumba yote ya kihistoria yatabakia kwenye mikono ya serikali ili kulinda utamaduni na urithi wa dunia.

“Kuanzia leo maombi hayo yatatangazwa awamu kwa awamu mpaka pale tutakapoona Mji Mkongwe unaimarika katika majengo na miundombinu yake na kuendelea kuwa kivutio bora cha wageni nchini mwetu”, alisema.

Sambamba na hayo, Waziri Lela aliwataka wawekezaji wazawa kujitokeza kupeleka maombi ili kupatiwa nafasi hiyo na kapewa ruhusa ya kufanya ukarabati.

“Kwa mara ya kwanza maombi yataanza kupokelewa Juni 21 hadi Julai tisa, maombi hayo yatakuwa ya kukodishwa kwa kuwekeza katika Mji Mkongwe iwe kwa mtu au kampuni lengo kuhakikisha ufanisi wa uhifadhi wa Mjimkongwe unapatikana haraka,” alisema.

Akizungumzia kuhusu nyumba ambazo zinataka kufanyiwa ukarabati, Waziri Lela alisema zaidi ya nyumba 127 ambazo zinahitaji kufanyiwa matengenezo ili ziwe katika hali ya ubora na kuvutia na nyumba 36 hazistahiki kuishi kutokana na ubovu.

Kuhusu changamoto zilizojitokeza kwa nyumba za Mji Mkongwe Waziri huyo wa habari alisema kufanyika kwa nyufa hali inayoweza kusababisha kuporomoka na kuleta maafa mengine kwa wakaazi wanaoishi katika nyumba hizo.

Waziri Lela akigusia kuhusu vipaumbele kwa Wizara hiyo alisema kufanya utafiti wa kujua uwezo wa visiwa vya Zanzibar wa kuhimili uwezo wa wageni wanaoingia na kuweza kuwahudumia pamoja na kutoa elimu juu ya dhana ya utalii kwa wote kwa wazawa na watu wote kwa kila rika hasa sehemu za uwekezaji.

Waziri huyo alisema kipaumbele chengine ni kuuendeleza usafi wa vivutio vya utalii kwa kuendeleza usafi kwa mashirikiano na kamati za mikoa na wilaya, vyuo vikuu na vikosi vya ulinzi na usalama.

Alibainisha kwamba kipaumbele chengine ni kuutangaza utalii wa Zanzibar kwa kushiriki katika matamasha ya kitaifa na kimataifa kwa kuhamasisha nchi jirani, na mikoa kufanya mikutano ya kikanda kuona ujio wa wageni unaongezeka sambamba na kuongeza pato la nchi.

Hata hivyo alisema kuifanyia ukaguzi miradi yote ya utalii ambayo inaendelea nchini ili kuona mapato hayapotei na kinachoingia kinafika serikalini.