NA MADINA ISSA

WAZIRI wa Utalii na Mambo ya Kale, Lela Mohamed Mussa, amewataka wanafunzi wa kidato cha sita waliohitimu Skuli ya Dk. Salmin Amour Juma, kujituma zaidi katika kusoma kwa ajili ya ufanisi ili waweze kupata maendeleo.

Akizungumza katika mahafali ya kwanza ya skuli hiyo huko Chumbuni banko, katika mahafali ya kwanza, ambapo alisema  hatua hiyo itaweza kuwasaidia katika kuimarisha maisha yao pamoja na kuisaidia serikali katika kupata watendaji wasomi.

Alisema serikali imekuwa ikitilia mkazo suala la Elimu kwani itaweza kuwasaidia wananchi kuwa na ufahamu sambamba na kujituma katika kujipatia kipato chao cha kila siku bila ya kutegemea fedha ya mtu.

Hivyo, Waziri Lela, aliwataka wanafunzi hao kutoridhika na walipofikia na badala yake kuendelea kupambana na suala la Elimu kwa kuhakikisha wanajiendeleza zaidi.

Sambamba na hayo, alifahamisha kuwa miongoni mwa mambo ya msingi kwa mwanadamu ni kuona wanapata Elimu, hivyo serikali itaendelea kuwatimizia wananchi wake mahitaji ya msingi ikiwemo Elimu bure.

“Serikali ya awamu ya nane inayoongoza Dk. Hussein Ali Mwinyi, imekuwa na lengo la kuwajali wananchi wake na ndio maana imekuwa ikiwahimiza kufanya kazi pamoja na kujiendeleza kielimu ili taifa liendelee kuwa na watu makini na wenye uwezo hivyo nanyi wanafunzi mujitahidi kujiendeleza kielimu” alisema.

Mapema, Mwalim mkuu wa skuli hiyo, Ramadhan Juma Hassa, alisema, Skuli hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo, upungufu wa vifaa vya kusomeshea masomo ya sayansi uhaba wa walimu, komputa hali inayowawia vigumu wakati wa ufundishaji na kudumaza kiwango cha ufaulu.

Akisoma risala ya wahitimu hao, Siti Kassim, alisema licha ya mafanikio waliyoyapata katika skuli yao ila wamekabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa baadhi ya vifaa katika lebo yao jambo ambalo muda mwengine limekuwa likisabaisha kukosa kazi za vitendo.

Hivyo, aliomba serikali kupitia Wizara ya Elimu Zanzibar kulishughulikia suala hilo ili kuweza kuwaengezea uwezo wanafunzi hao kwa kusoma masomo ya sayansi zaidi.

Sambamba na hayo, wanafunzi hao, waliwapongeza wazazi, walezi na walimu wa skuli hiyo kwa mashirikiano yao wakati wote wakiwa skuli na kuwataka kuendelea kudumisha ushirikiano, ili skuli iweze kutoa matokeo mazuri zaidi.

Jumla ya wanafunzi 100 wa Skuli ya Dk. Salmin Amour Juma  walihitimu kidatu cha sita ambapo skuli hiyo ilianzishwa mwaka 2019 ikiwa na wanafunzi 114 wa masomo ya sayansi