NA HAFSA GOLO
WAZIRI wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Abdallah Hussein Kombo, anatarajiwa kuwa mgeni rasmin katika kongamano la maadhimisho ya siku ya mabaharia Duniani.
Mkurugenzi Uhusiano wa Mamlaka ya Usafiri Othman Said Othman, alieleza hayo wakati alipokuwa akizumgumza na gazeti hili ofisini kwake Malindi mjini Unguja.
Alisema kongomanao hilo litafanyika ukumbi wa shekhe Idrissa Abdulwakili Kikwajuni Juni 20, mwaka huu na kujadili mambo mbali mbali muhimu ambayo yatasaidia katika kuimarisha utekelezaji wa uchumi wa buluu na yenye kuleta maendeleo nchini.
Aidha alisema Mamlaka ya Usafiri Baharini (ZMA), imekusudia kuleta mageuzi ya kiutendaji kwa mabaharia hao ili wawe ni sehemu ya kuitangaza Zanzibar vyema wakati wanapotekeleza majukumu yao ndani na nje.
Hata hivyo alisema, ZMA imejipanga kuunga mkono juhudi za serikali katika uimarishaji wa uchumi wa buluu ambapo katika kongomano itatoa fursa kwa wadau kujadili na kutafakari namna bora ya kutumia mabaharia hao kwa maslahi ya Taifa na kuwa ni miongoni mwa sehemu ya kuleta chachu katika uchumi wa buluu.
Pamoja na hayo alisema,katika kongomano hilo kutakuwa na maonesho yatakayofanywa na baadhi ya taasisi zinazohusiana na masuala ya mabaharia.
Aidha alisema Shirikisho la mabaharia duniani IMO huadhimishwa kila mwaka mwezi Juni 25 na kauli mbiu yam waka huu ni “Fair future for seafarers”.
Mapema mmoja wa mabaharia Nassour Juma,wakati akizungumza na gazeti hili, alisema Zanzibar kipo Chama cha Mabaharia na kina hazina kubwa ya watendaji wenye uwezo na upeo wa kuandaa mikakati ambayo yatasaidia kutumia fursa za maendeleo zilizomo katika Shirikisho la Kimataifa la Wafanyakazi Duniani (ITF) kwa ajili ya Zanzibar.
Pia alisema,chama hicho kimekuwa na mambo mengi muhimu yaliopatikana kupitia shirikisho hilo ambayo yanaweza kuimarisha sekta ya usafiri na kuleta mafanikio.
“Wakati watendaji wa chama hicho wanapohudhuria katika mikutano ya Kimataifa,kisera,kanuni za Kimataifa pamoja na utetezi wa mabaharia wamekuwa wakijifunza fursa nyingi za kiuchumi ambazo zinaweza kuleta chachu ya mabadiliko nchini,”alisema .
Hivyo alisema iwapo serikali itakaa pamoja na chama hicho upo uwezekano kwa serikali kutumia fursa mbali mbali, ikiwa ni pamoja na usajili wa meli za nje zilizosajiliwa na Mamlaka ya Usafiri wa Baharini (ZMA) sambamba na vijana wazalendo kutumia fursa za ajira.
Alisema hatua hiyo itasaidia kutatua changamoto zinazojitokeza katika sekta ya bahari kutumia chama hicho ambacho kinatambulika kisheria ndani na nje.