Mabodi: Rais Samia ni chuma cha pua, aliyejipambanua kuwahudumia Watanzania ndani ya siku 100 za uongozi wake.

Ameweka kando ukanda, udini, ukabila, ujimbo na kuwaunganisha Watanzania kuwa kitu kimoja, huku silaha kuu ikiwa ni kusimamia haki na kuleta  maendeleo kwa taifa.

Na Isi-haka  Omar, Zanzibar.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan  ametimiza siku 100 Ikulu huku akielezwa kuwa kiongozi shupavu anayeonyesha dhamira ya wazi ya kuwatumikia Watanzania kwa kuboresha nyanja mbalimbali zikiwamo miundombinu ya usafiri, maji, afya, elimu na umeme.

Rais Samia  aliapishwa Machi 19, 2021 kushika hatamu ya kuongoza nchi kufuatia kifo cha mtangulizi wake hayati John Magufuli aliyefariki Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena , Kijitonyama , Dar es Salaam.

Akizungumzia siku 100 za uongozi wa Rais huyo wa kwanza mwanamke, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Zanzibar, Abdallah Juma Saadala ‘Mabodi’, anasema   dhamira ya Rais Samia kuwatumikia wananchi bila kuchoka imeonekana tangu awali alipoapishwa kuongoza nchi.

Anasema hii inatokana na uzoefu mkubwa alioupata kutoka katika uongozi wa Serikali ya awamu ya tano iliyokuwa ikiongozwa na hayati  Dk John Magufuli  imempa na kumpa umahiri na nguvu za kiutendaji , ukakamavu, ufanisi na weledi mkubwa wa kuongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Anasema ndiyo maana amejipambanua katika uongozi kwa kuangazia utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwamo ya kimkakati kuanzia ngazi ya

Serikali za Mitaa hadi Taifa kwa ujumla.

“Huku akiongozwa na sera, dira na ilani ya uchaguzi ya CCM, Rais Samia, mara moja ameendeleza vile vilivyoanzwa na mtangulizi wake kwa kuhakikisha ikiwa ni pamoja na kusema bayana kuwa miradi yote iliyoachwa na Magufuli ikamilike kwa wakati na kutofanya hivyo ni laana kwa Taifa”anasema na kuongeza.

“Hii inamaanisha moja kwa moja alikuwa anatembea mguu mmoja na mtangulizi wake katika maamuzi mbalimbali ambayo sasa anakwenda kuyakamilisha, huku akiongeza na ubunifu wake kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa”anasema Mabodi.

Mabodi anafafanua kuwa “ Mhe Rais Samia amezitumia siku 100 kuonyesha kuwa kuongoza  nchi ni dhima kubwa kwa Mwenyezi Mungu na deni kubwa kwa wananchi walioahidiwa kutendewa mema na Serikali yao, hivyo uadilifu wa kuwatendea haki ni jambo lisilokwepeka kwa Watanzania wote bila kujali  dini, kabila, rika wala jinsia.

“Kila mmoja anaona Rais Samia alivyo na moyo wa ulezi kwa Watanzania, ndio maana wakati wote anahubiri amani, utulivu, mshikamano na uendeshaji wa Serikali juu ya utawala bora kwa wananchi na utendaji uliotukuka”anasema.

Anasema akiongozwa na dhamira ya ulezi kama mama na uongozi wenye weledi  hata alipoingia madarakani alifanya mabadiliko madogo ya baraza la mawaziri na wakuu wa mikoa  na kugusa makundi yote wakiwamo wanawake kulingana na alivyoona watamsaidia kutatua changamoto kwa wananchi na kujenga uaminifu kwa Serikali huku akiwapa.nafasi vijana ya kuongoza kwenye wilaya mbalimbali nchini.

“Kuwapa nafasi vijana katika uongozi maana yake nini? Kwa kiongozi makini jibu ni rahisi tu, anachofanya ni kuandaa viongozi wa baadaye watakapoendelea wanapoishi wazee wanaoongoza sasa, lakini wakiwa wameiva kisiasa na kiuongozi kwa sababu waliandaliwa tangu wakiwa vijana” anasema Mabodi.Hakuishia hapo bali maelekezo yanayotokana na mwongozo wa Serikali aitakayo aliyoyatoa wakati akilihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Aprili 22, 2021, ndiyo mwelekeo wa bajeti ulivyo.

“Bajeti haikuwasahau vijana wanaojiendeleza kielimu ambapo Serikali ya Samia imejipambanua vizuri kwenye bajeti iliyotangazwa ndani ya siku 100 za mama Samia madarakani mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, elimu msingi bila ada, uimarishaji wa vyuo vya ufundi stadi, kukuza ujuzi kwa vijana na ujenzi wa miundombinu ya elimu zimetengwa Sh406.6 bilioni”anasema Mabodi.

 Umahiri wake ndani ya chama:

Licha ya kufanya mambo mengi ya kitaifa wakiwa ni kiongozi namba moja wa nchi, pia katika chama chake anakubalika kutokana na namna anavyochapa kazi.

“Kutokana na utamaduni wa CCM Rais ndiye anayekuwa mwenyekiti wa chama hivyo tulikaa kupitia Mkutano Mkuu Maalumu akachaguliwa kwa kura nyingi kuwa mwenyekiti wetu” anasema Mabodi na kuongeza.

“Msemo wake wa kazi iendelee anamaanisha alikuwemo ndani ya Serikali na anavyovifanya sasa baadhi walivipanga na mtangulizi wake hayati Magufuli, yeye akiwa Makamu wa Rais, hivyo anavyovifanya sasa katika nafasi ya urais ni mwendelezo” anasema.

Anasema hata bajeti imeandaliwa kwa kuzingatia nini Rais anataka kifanyike ikiwamo kuzingatia nyaraka na miongozo mbalimbali ikiwemo. Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano 2021/22 – 2025/26 ambao umeandaliwa kwa kuzingatia dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 – 2025, Dira ya Maendeleo ya Afrika Mashariki 2050,Ajenda ya Maendeleo ya Afrika 2063,Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030,Mwongozo wa Ushirikiano wa Maendeleo na makubaliano mengine ya kikanda na kimataifa ambayo Tanzania imeyaridhia.

Anasema ndiyo maana anazisimamia vema kazi za miradi ya Serikali chini ya Chama Cha Mapinduzi iliyokuwa imeanza kutekelezwa ikiwamo ya kusambaza umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambayo zitatumika takribani Sh1.02 trilioni, Ujenzi na ukarabati wa reli ikiwemo ujenzi wa reli kwa Kiwango cha kimataifa zimetengwa Sh1.49 trilioni, Ujenzi wa barabara, madaraja, na viwanja vya ndege Sh 1.15 trilioni na usimamizi wa miradi yote ya kimkakati.

“Hii yote ni kuhakikisha anasimamia vema ilani ya chama na anatimiza ahadi za wananchi kama ambavyo alifanya wakati akimuombea kura mtangulizi wake na baadaye kushika hatamu ya kuongoza nchi.

“Siku 100 za Rais Samia zimeonyesha ana nia ya dhati ya kutekeleza kila alichokiahidi kwa kusimamia misingi, dira, mwongozo na maelekezo ya CCM”anasema Mabodi.

Mabodi anasema Rais Samia anasimamia kwa nguvu zote na kuhakikisha inamalizika kwa ufanisi na viwango. Lengo ni kuivusha Tanzania  kuja juu kutoka nchi yenye kipato cha  kati  daraja la chini na kwenda kipato kati cha daraja ya juu.

MASUALA YA FEDHA:

Anasema katika bajeti ya anayoisimamia ya mwaka 2021-2022, ambayo ni Sh…inagusa maisha ya makundi yote katika jamii , iliyozingatia vipato na mahitaji yao.

“Mfano Kodi zimeongezwa lakini kulinda viwanda na uzalishaji wa ndani ili kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa ndani, lengo ni kuwanufaisha wananchi wa kipato cha chini waweze kuja juu, wapate maisha rahisi na waondokane na madhila  yatokanayo na huduma zisizofikika kwa haraka au kuongeza tija za uwekezaji mdogo”.

Mabodi anasema kupitia Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano Dk Mwigulu Nchemba  alisema wazi kuwa Rais ataziimarisha barabara za ndani ambazo zinamsaidia mwananchi wa chini hasa wanawake kuondokana na adha ya kujifungulia njiani kutokana na ubovu wa barabara hivyo kupata shida ya kufika katika vituo vya afya, kuwawezesha wanafunzi kufika haraka mashuleni na wakulima wanaosafirisha bidhaa zao kuzifikisha sokoni zikiwa katika ubora unaokusudiwa.

Anasema Rais ameweka mikakati ya kuhakikisha fedha za bajeti zinatumika ipasavyo na kwa maslahi ya Watanzania ikiwamo kulinda usalama wa afya zao kwa kujenga   hospitali  na zahanati.

Katika suala la kuboresha afya ya wananchi kwa usimamizi na mwongozo wa mama Samia, ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi pamoja na ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya afya  zimetengwa Sh265.8 bilioni.

lakini  pia kuwatizama wafanyabiashara ndogo ndogo wakiwemo Wamachinga , mama lishe na baba lishe , na baadhi ya bidhaa zimepunguzwa kodi kwa lengo la kumtizama mwananchi wa kipato cha chini ili kumkwamua kutoka katika umasikini.

KUSIMAMIA HAKI

Anasema mapema kabisa Rais Samia aliueleza umma na viongozi aliowateua katika Serikali yake wakiwamo wenye jukumu la kukusanya kodi kuwa fedha anazitaka zikusanywe lakini siyo za dhuluma na alikemea suala la kubambikia watu kesi na kufanya Mahakama ambayo ni chombo cha kutoa haki kuwa sehemu ya kukusanyia mapato.

“Juzi amesimamia kutolewa kifungoni kwa viongozi wa dini wakiwemo masheikh wa Uamsho. Huo ni ushahidi tosha  kuwa  mtu anayeamini amani kwa kusamehe na kuona  yaliyopita si ndwele iliyobaki tugange  yajayo” anasema na kuongeza.

“Pia kuna wananchi wengine waliokuwa wamewekwa ndani kwa makosa na tuhuma mbalimbali ambao ushahidi wao ni wa kusuasua amewasamehe na kuachiwa huru kwa lengo la kujenga Taifa moja lenye maendeleo” anasema.

Mabodi anampongeza Rais Samia kwa kusema, “Nampongeza yeye pamoja na  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi, kwa kukubali maridhiano ya kitaifa ambayo lengo lake ni kutengeneza nchi moja yenye mwelekeo mmoja ambao unatembea katika reli iliyokuwa safi, japokuwa tuna tofauti za kiitikadi, kimaono na kisera lakini jambo kubwa ni kuwaondoa wananchi katika chuki na siasa za utengano”.

DIPLOMASIA

Mabodi anasema Rais Samia ameonyesha ukomavu wa hali ya juu katika masuala ya kidiplomasia kuanzia kwa mabalozi aliowachagua kuiwakilisha nchi nje ya mipaka hadi namna anavyoshirikiana na mataifa mbalimbali ikiwamo kwenda na kuwakaribisha wao kuja nchini.

Anasema katika siku hizi 100 Rais Samia, ameonyesha kutokuwa na ubaguzi wa kidini na kikanda kwanikatika teuzi zake mbalimbali amekuwa akiteua kutokana Zanzibar.

” Hili jambo linaonyesha kuwa ni Rais wa wote na lengo ni utanzania na wala si ujimbo au uzawa, jambo hili limekuwa likitokea mara chache japokuwa katika CCM lipo watumishi wake wanatoka sehemu zote za Muungano wa Tanzania”.

“Ndani ya siku 100 tangu aingie madarakani amejenga uaminifu mkubwa kimataifa ambapo ameshiriki vikao vya Jumuia ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na kutembelea nchi mbalimbali na yeye kualika marais wenzake wa mataifa mbalimbali kwa ajili ya kujenga mahusiano ya nchi za nje na zile rafiki.

Anasema Rais Samia katika siku 100 ameonyesha kusimamia vizuri sera za ndani ya CCM, Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020/2025 kuna masuala Diaspora  na Uchumi wa Bluu(Blue Economy) kama vile mito,maziwa,bahari na n.k  awali hayakuwepo kwa sasa  ameyapa kiaumbele katika  mambo muhimu ya kuimarisha uchumi wa nchi akieleza  ni namna gani kunaweza kuibuliwa ‘uchumi wa blue’ ukajalizwa katika uchumi wa kijani na pakapatikana  maendeleo barani Afrika na Tanzania  kwa ujumla.

” Mfano  namna anavyojali masuala ya Muungano, amenunua boti 8 ambapo 4 kati ya hizo ni kwa ajili ya upande wa Zanzibar na zingine Tanzania Bara.

“Kwa kuwa amewahi kuongoza katika Taasisi ya Muungano anajua vizuri changamoto na kero zote za Muungano na matumaini yetu atazimaliza kidogo kidogo” anasema.

AONYESHA DHAMIRA YA KUWATUMIA WANANCHI BILA KUCHOKA.

Anasema Rais  Samia hapumziki ni chuma cha pua anafanya kazi usiku na mchana unajua kweli kuwa huyu ni ‘TANZANITE WOMAN’ sasa wanawake kama wanataka ile 50 kwa 50,  wamepata mfano wa kuiga.

Umakini:

Anasema ndani ya siku 100 Rais ameonyesha umakini mkubwa has a katika kusimamia na kulinda rasilimali za nchi ikiwamo madini, anajitahidi kuhakikisha kinachopatikana kinatumika kwa manufaa ya nchi.

Anafafanua pia kiongozi hiyo wa juu wa nchi anakemea na kufuatilia kila jambo kwa umakini na kuonya kwa njia ya upole hasa pale anapokuwa akisimamia jambo lenye maslahi mapana na nchi  na haogopi kufanya maamuzi magumu.

“Tukiangalia na kutathmini kwa upana zaidi siku 100 za Rais  Samia najivunia ndani ya CCM kuwa tumepata Mwenyekiti mahiri atakayetuvusha salama katika kutekeleza mwongozo wetu ambao ni Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020/2021 pamoja na dira  ya Serikali ya kuleta maendeleo endelevu nchini” anasema.

Mabodi anasema “Nilieleza pamoja na kuwa na sifa za uongozo zinazoonekana bayana katika utendaji wake ndani ya siku 100, pia ni mlezi ambapo anahakikisha kila sekta inakuwa sawa”anasema.