NA ALI SHAABAN JUMA

 MACAO ni kisiwa kilichopo kusini mashariki mwa China chenye ukubwa wa kilomita za mraba 22.  Kisiwa hicho kina urefu wa kilomita 12 kutoka kaskazini hadi kusini na upana wa kilomita saba kutoka mashariki hadi magharibi. Kihistoria kisiwa cha Macao chenye watu 658,000 ni sehemu ya China ambacho kilitawaliwa na Wareno.

Katika mwaka 1553, wakati Wareno wakifanya misafara mbalimbali ya baharini, walitia nanga katika kisiwa hicho. Wafanyabiashara hao wa Ureno walivutiwa na mandhari nzuri ya kisiwa hicho na ndipo walipofanya ujanja wa kuhamia kisiwani humo.

Waliomba ruhusa ya kukaa kisiwani hapo kwa muda kwa madai ya kuanika bidhaa zao zilizoroa kutokana na dhoruba kali waliyokumbana nayo baharini. Wakati huo, China ilikuwa chini wa utawala wa Ming.

Katika mwaka 1845, serikali ya China chini ya uongozi wa Qing ilitangaza kuwa Macao ni bandari huru.  Lakini katika mwaka 1848, Wareno waliifunga bandari ya kisiwa hicho kwa nguvu na kuwafukuza maofisa wa serikali ya China waliokuwa kisiwani hapo.

Mnamo mwaka 1851, Wareno walikiteka kisiwa cha Taipa kilichopo kusini mwa Macao na katika mwaka 1864 wakoloni hao wa Kireno walikiteka kisiwa chengine cha Coloane na huo ukawa ndio mwanzo wa ukoloni wa Wareno katika visiwa hivyo. Baada ya mazungumzo ya muda mrefu kisiwa cha Macao kilirejeshwa mikononi mwa China hapo mwaka 1999.

Kwa karne kadhaa, kisiwa cha Macao ni maarufu kwa utalii duniani. Hali hiyo inatokana na hali nzuri ya hewa kisiwani humo, kuwepo kwa utamaduni mchanganyiko na bandari huru ambayo inatoa fursa kwa wafanyabiashara mbalimbali duniani kuingia na kuwekeza kisiwani humo.

Mbali ya hayo yote, Macao ni kituo kikuu cha kamari duniani ambapo hivi sasa mapato yatokanayo na michezo mbalimbali ya kamari kisiwani humo ni makubwa kuliko yale yanayopatikana huko Monte Carlo, Marekani mji ambao kabla ya hapo ulikuwa ndio kituo kikuu cha kamari ulimwenguni.

Kihistoria, mchezo wa kamari ulipata nguvu kisiwani Macao hapo mwaka 1872, baada ya wakoloni wa kiingereza kupiga marufuku mchezo wa kamari katika kisiwa cha Hong Kong na wakati huo huo serikali ya Qing ya China kupiga marufuku kamari katika jimbo la Guangdong.

Kutokana na marufuku hayo, wachezeshaji kamari walihamia katika kisiwa cha Macao na kuendesha biashara hiyo ambayo tayari ilikwishaota mizizi kisiwani humo.

Katika mwaka 1937, serikali ya Macao ilianzisha Casino za kamari kisiwani humo na kuzitoza kodi Casino hizo na kuongeza mapato ya kisiwa hicho. Hapo mwaka 1961, serikali ya Ureno ilihalalisha kamari kisiwani Macao na kuongeza idadi ya watalii na wachezeshaji kamari kisiwani humo.