NA FATMA KASSIM

WIZARA ya Afya Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto imewataka Madiwani Wilaya ya Mjini kuisaidia Wizara hiyo katika kukabiliana na kutokomeza malaria, ili kuweza kufikia lengo la serikali la kumaliza malaria ifikapo 2023.

Akizungumza na Madiwani hao, Mkurugenzi Idara ya Kinga na Elimu, Dk. Fadhil Mohammed Abdalla, amesema ni wakati wao sasa kwa Madiwani hao kushuka kwa wananchi

kuwapatia elimu ya kukabiliana na malaria, ikiwa ni pamoja na usafi, kuondoa madimbwi ya mazalia ya mbu katika makazi yao.

Amesema madiwani wanadhima kubwa katika kuifikia jamii kwenye wadi zao na mashirikiano ya pamoja na taasisi tofauti itaweza kuondoa maraadhi hayo kama serikali ilivyoweza kutokomeza maradhi mengine yakiwemo polio.

Nae Mstahiki Meya Baraza la Manispaa ya Mjini,  Ali Haji Haji, amewataka wakaazi wa maeneo hayo kutumia vyandarua vilivyowekwa dawa na kuweka usafi katika maeneo yao, ili kupambana na maradhi hayo

Amesema kupitia juhudi zinazofanywa na Baraza la Manispaa ya mjini ya kuweka mji safi ni njia moja wapo ya kupambana na maradhi tofauti yakiwemo ya malaria kwa kuondoa mazalia ya mbu.

Nao, Madiwani hao wamesema kupitia elimu waliopatiwa kupitia kitengo cha malaria kama kamati ya huduma za jamii ni wajibu wao sasa kushuka katika jamii na kuhamasisha wananchi kujikinga na malaria katika kuelekea katika msimu wa mvua zinazotarajiwa kunyesha baadae.