ZASPOTI.
VIJANA wameshauriwa kushiriki katika michezo mbali mbali kutokana na kuwa hivi sasa ajira zinapatikana kupitia sekta hiyo.
Ushauri huo umetolewa na Mwakilishi wa Kwahani, Yahya Rashid Abdalla ‘Mamba’ wakati alipozungumza na wachezaji kwenye mechi ya kirafiki kati ya Mafunzo na Wabunge kutoka nchini Kenya juzi.
Alisema, awali michezo ilikuwa ni moja ya burdani na starehe, lakini, hivi sasa imekua ajira hivyo ni vyema vijana kutumia fursa hiyo katika kujiletea maendeleo yao binafsi.
“Michezo tulikua tunaona ni burudani, lakini, pia ni afya, sasa ni tofauti na michezo ni ajira, mkiitumia inavyotakiwa mtafanikiwa katika maisha yenu”, alisema.
Aidha, alisema, serikali imekua mstari wa mbele katika sekta ya michezo ili kuwasaidia vijana kukuza vipaji vyao, hivyo, aliwataka vijana hao kuzitumia fursa hizo zinazotolewa ili kufika mbali na kuitangaza nchi kitaifa na kimataifa .
Kuhusu ziara ya Wabunge hao kutoka Kenya, alisema, ina dhamira ya kuendeleza uhusiano waliokuanao hususan wa kimichezo.
Alisema ujio wao ni faraja kubwa kwani unajenga uhusiano mzuri ambao utakua chachu ya maendeleo katika nchi hizo mbili.
Wabunge wa Kenya wapo nchini kwa ziara ya wiki moja ya kimichezo.