NA HASHIM KASSIM

MKUU wa Idara ya habari na mawasiliano ambaye pia ni msemaji wa klabu ya Simba Sc Haji Manara, amesema  michezo ni chanzo cha mtoto kuwa na akili nzuri.

Aliyabainisha hayo wakati alipokuwa katika bonanza la michezo ya watoto lililoandaliwa na Leera School ambalo lilifanyika katika uwanja wa Amaan.

Manara alieleza kuwa michezo ina umuhimu mkubwa kwa watoto, kwani mara nyingi mtoto anayeshiriki katika michezo kikamilifu hufanya vizuri katika masomo.

“Wataalamu wengi Duniani wamethibitisha kuwa watoto wanaoshiriki michezo wanakua na maarifa mengi darasani kwa sababu akili yao na miili yao imechangamka” alisema Manara.

Pia aliongeza kuwa kufanya mabonanza hasa ya michezo maskulini ni jambo jema na kuwataka walimu wa skuli ya Leera kuendeleza utamaduni huo kwani ni jambo jema.

Msemaji huyo alisema michezo ni sehemu ya ajira hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kuithamini ndio maendeleo na msingi wake ni watoto walioko maskulini.