NA HAJI NASSOR, PEMBA
TAASISI ya ‘Search for Common Ground’ ofisi ya Pemba, imewataka watatuzi wa migogoro, kutumia umakini mkubwa wakati wanapotatua migogoro ikiwemo ya kisiasa, ili kuhakikisha kila upande unaridhika.

Kauli hiyo imetolewa na Afisa Msaidizi wa Mradi wa mradi wa ‘Dumisha Amani Zanzibar’ kwa upande wa Pemba Khamis Abass Khamis, alipokuwa akiwaelezea Maofisa wa serikali na watendaji wa serikali ngazi za mitaa, kwenye mafunzo ya siku tatu, yaliyofanyika ukumbi wa Maktaba Chake chake.

Alisema, moja ya sharti kubwa kwa mtatuzi wa mgororo, ni kuwa na utamaduni wa kusikiliza pande zote husika kwa umakini, kuheshimu utamaduni wao pamoja na lugha, ili uamuzi utakapotoka usiwe na shaka kwa wahusika.

Alisema kuwa, umakini wa msuluhishi siku zote, ndio unaoweza kuchangia kutatu migogoro katika jamii, ambapo sifa hiyo ikikosekana kwa msuluhishi huyo, ni vigumu kufikia malengo yaliokusudiwa.

“Zipo sifa kadhaa anazotakiwa kuwa nazo msuluhishi yeyote yule, hata kama mgogoro unaonekana ni mdogo au mkubwa, maana ukipoteza sifa hiyo, huwa vigumu kutatua mzozo,’’alifafanua.

Katika hatua nyingine, Afisa huyo alisema sifa nyingine anazopaswa kuwa nazo msuluhishi ni kuwajua wahusika wa mgogoro, chanzo pamoja na athari zake.

Mapema Afisa Habari kutoka tasisi ya Search for Common Ground Zanzibar, Khelef Nassor Rashid, alisema jamii ya Zanzibar imekuwa ikiingia katika migogoro kila baada ya kumalizika kwa shughuli ya uchaguzi mkuu, jambo linalopoteza sifa ya visiwani hivi.

Alifafamisha kuwa, ndio maana tasisi hiyo ya ‘SFCG’ imeona vyema kutafuta mradi maalum wa kutoa elimu kwa wazanzibari, juu ya mbinu za kujikinga na kutatua migogoro.

“Nadhani sasa mradi huu unaweza kuwa mwarubaini kwetu sisi wazanzibari ya kutokutumbukia kwenye siuntafahamu ya wenyewe kwa wenyewe, kunakosababishwa na siasa,’’alieleza.

Aliwaeleza washiriki wa mafunzo hayo kuwa, wazanzibari wanautamaduni wao wa kuishi kwa kusaidiana, kuishia pamoja, kuvumilia, kupendana tokea asili, sasa sio vyema siasa kuwagawa.

“Mradi huu wa ‘Dumisha amani Zanzibar’ unataka kuona kuwa Zanzibar baada ya uchaguzi na hata kabla hatuingii tena kwenye mizozo ambayo tija yake haionekani,’’alieleza.

Shuwena Hamad Ali kutoka ofisi ya Mkuu wa mkoa wakaskazini Pemba, alisema sasa amepata elimu ambayo, kwa muda mrefu alikuwa akiihitaji ili kufanya kazi kwa ufanisi.