NA ASYA HASSAN

MKUU wa Wilaya ya Kati, Marina Joel Thomas, amewataka vijana waliopatiwa Mafunzo na taasisi ya PDS kuyatumia vizuri, ili waweza kujikwamua na hali ngumu ya maisha.

Akiwakabidhi vyeti wahitimu wa Mafunzo hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, alisema katika kupunguza tatizo la ajira kwa vijana ni vyema kuyatumia vizuri Mafunzo waliopatiwa kwa kuyafanyia kazi.

Alisema serikali kupitia wadau wa maendeleo imekusudia kuwakwamua vijana kupitia fursa mbali mbali zikiwemo za ujasiria mali, hivyo amewataka kuzitumia vyema ili ziweze kuwanufaisha na kuleta tija kwao na taifa.

Marina alitumia fursa hiyo kuwataka vijana kutojihusisha na masuala ya uvunjifu wa amani pamoja na matumizi mabaya ya dawa za kulevya, kwani kufanya hivyo kutapelekea kuvuruga mfumo mzima wa maisha wako.

Mkurugenzi kutoka Idara ya Maendeleo ya Vijana Zanzibar, Shaibu Ibrahim Mohammed, alisema serikali imejipanga kupunguza tatizo la ajira kwa vijana kupitia taasisi mbalimbali ikiwemo PDS, ili kuenda sambamba na dhamira ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi la kuwapatia ajira vijana.

Katibu Mtendaji wa PDS, Mohamed Nassor Yussuf, alisema taasisi hiyo inalengo la kuwakwamua vijana na kupunguza umaskini kwa kuwapa elimu ya ujasiriamali itayowasaidia kujipatia kipato chao na familia zao.

Nao washiriki wa Mafunzo hayo walisema watayatumia vyema na kuwataka vijana wenzao kujihusisha na shughuli za kimaendeleo na kuachana na dhana ya kusubiri ajira kutoka serikalini.

Hata hivyo walitumia fursa hiyo kuwataka vijana wengine waliokuwa hawana ujuzi kwenda kujifunza ujuzi wa fani mbalimbali kupitia taasisi hiyo, ili waweze kujitegemea wenyewe.