NA MARYAM HASSAN

MKAAZI wa Kijini Makunduchi, anayekabiliwa na kesi ya kuvunja nyumba kwa dhamira ya kutenda kosa, amepelekwa rumande baada ya kushindwa kukamilisha masharti ya dhamana.

Mshitakiwa huyo ni Yussuf Mohammed Ali (27), amepelekwa rumande na mahakama ya mkoa Mwera hadi Juni 14 mwaka huu, kesi yake itapoanza kusikilizwa ushahidi.

Awali, Hakimu wa mahakama hiyo Said Hemed Khalfan, alimtaka mshitakiwa huyo kusaini bondi ya shilingi 500,000 pamoja na kuwasilisha wadhamini wawili, wenye na vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi pamoja na barua za Sheha wa Sheia wanazoishi, ambao kila mmoja atasaini bondi ya kima hicho hicho cha fedha.

Mshitakiwa baada ya kupewa masharti hayo alishindwa kuyatekeleza na kupelekea kupelekwa rumande hadi Juni 14 mwaka huu.

Mapema, Mwendesha Mashitaka Ayoub Nassor Shariff, Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), alidai kuwa mshitakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo kwa kosa la kuvunja nyumba kwa dhamira ya kutenda kosa la wizi.

Kosa hilo anadaiwa kulitenda Disemba 27 mwaka jana majira ya saa 8:00 za mchana huko Makunduchi Kigaeni, wilaya ya Kusini mkoa wa Kusini Unguja.

Mshitakiwa huyo anadaiwa kuwa, siku hiyo alivunja nyumba na kuingia ndani inayomilikiwa na Zsigmond Eros, kwa dhamira ya kutenda kosa la wizi ndani humo.

Akiwa ndani humo, mshitakiwa huyo anadaiwa kuiba CCTV camera 3 zenye thamani ya shilingi 360,000 mali ya Zsigmonda Eros, jambo ambalo ni kosa kisheria.

Aliposomewa kosa lake hilo, mshitakiwa huyo alikataa na kuiomba mahakama kumpa dhamana, jambo ambalo lilikubaliwa na upande wa mashitaka kwa kuwa kosa hilo linadhaminika.

Aidha Wakili huyo wa serikali, aliiomba mahakama kuiahirisha shauri hilo na kupangwa terehe nyengine kwa ajili ya kusikilizwa ushahidi, kutokana na upelezi wake tayari umeshakamilika.