NA HAMISUU ABDULLA

HATIMAYE viongozi wawili waandamizi wa Jumuiya za Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI), Sheikh Farid Hadi Ahmed na Mselem Ali Mselem waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya ugaidi wameachiwa huru.

Hapo jana majira ya asubuhi habari za kuachiliwa kwa masheikh hao zilizagaa mitandaoni, huku baadhi ya magurupu ya mitandao ya kijamii yakichapisha picha wakiungana na familia zao.

Picha mbalimbali zilisambaa mitandaoni wakionekana masheikh hao na wakiwa na ndugu zao. Wanasiasa mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii, wameonekana kuunga mkono hatua ya kuachiwa huru viongozi hao wa dini.

Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Sylvester Mwakitalu hapo jana alinukuliwa akisema kuwa masheikh wote 36 waliokuwa wakikabiliwa na tuhuma hizo wameachiliwa huru na kilichobaki sasa ni taratibu za kutoka gerezani.

“Ni kweli wameachiwa huru. Nimewafutia wote mashtaka yaliyokuwa yanawakabili. Sasa suala la kutoka gerezani kama wameshatoka wote au wangapi hilo ni suala la taratibu za Magereza, lakini mimi nimewafutia mashitaka wote”, alisema.

Mmoja wa mawakili wa masheikh hao, Abdallah Juma mbali na kuthibitisha kuachiliwa huru na yeye kuwaona. “Nimewaona wawili wameachiwa huru na nimekwenda kuwatembelea baada ya Jamhuri kuonyesha nia ya kutoendelea na kesi”, alisema wakili huyo.

Masheikh hao waliokuwa wanashikiliwa gerezani kwa makosa ya ugaidi, walifunguliwa kesi hiyo namba 29 ya mwaka 2014 wakikabiliwa na mashtaka ya kuwaingiza watu nchini kushiriki vitendo vya ugaidi, kusaidia na kuwawezesha kufanyika vitendo hivyo.

Wakizungumza na waandishi wa habari walisema kuwachiwa kwao huru kunanatokana na shindikizo la viongozi akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi   ambazo zimepelekea kuwa pamoja na familia zao.

Sheikh Farid Hadi Ahmed alisema Rais Samia sio mama wa taifa bali ni mama wa Afrika na amekimbilia kujiepusha na mzigo mkubwa kwa mwenyezimungu ambayo ni zulma.

Hata hivyo aliwaomba viongozi kuendelea kutumia busara zao kwa kuwaokoa watu wengine ambao wamewekwa gerezani kwa muda mrefu bila ya kesi zao kusikilizwa na kutolewa hukumu.

“Pale gerezani kuna watuhumiwa wapatao 220 ambao kesi zao hazijasikilizwa na sheria hazijafuatwa mfano yupo mzee wa miaka 96 yupo pale anatuhumiwa kwa kesi ya ugaidi tunaiomba serikali itumie busara ipitie kesi zao”, alisema.

Kwa upande wake Sheikh Mselem Ali ambae ni miongoni mwa walioachiwa aliwapongeza viongozi hao ambao wameonesha dhahiri kuwa wapo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi.

Aliwataka wananchi watulie na furaha yao itoshe kuwa wapo huru na kuendelea kuhubiri amani ya nchi ili kuona Tanzania ikiwemo Zanzibar inabaki kuwa na amani.

Hivi karibuni Mufti wa Tanzania na viongozi mbalimbali wa dini wameongeza shindikizo la kutaka kesi za viongozi dini waliokuwa magerezani zimalizike.

Washtakiwa hao walikuwa wanadaiwa kujihusisha na makosa ya ugaidi kinyume na kifungu cha 27(c) cha sheria ya kuzuia ugaidi ya 2002 Januari 2013 na Juni 2014.

Awali walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Dar es Salaam kwa hatua za awali kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu kwa usikilizwaji kamili wakikabiliwa na jumla ya mashtaka 25.