HAFSA GOLO NA MOHAMMED RASHID, MCC
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Malum za SMZ, Masoud Ali Mohamed, amewahakikishia wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwamba serikali itaendelea kutatua changamoto zinazowakabili wananchi hatua kwa hatua.
Akijibu baadhi ya wajumbe wa baraza la wawakilishi kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya serikali ya mapinduzi Zanzibar kwa mwaka wa fedha 2021/2022, Masoud alisema ili kuhakiksha huduma bora kwa wananchi, watendaji wake watalazimika kwenda na kasi ya serikali ya awamu ya nane.
Alisema serikali haitafanya mzaha na watendaji wazembe na kwamba itaendelea kusimamia utatuzi wa changamoto zilizopo na zitakazojitokeza.
Aidha aliwashauri wajumbe kutoingilia mamlaka ya taasisi zenye wajibu wa kudhibiti vitendo vya rushwa na uhujumu uchumi ili zitekeleze majukumu yake kwa ufanisi.
Alibainisha kwamba awali zilikuwepo kasoro katika ukusanyaji wa mapato ya serikali katika Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) jambo lililochangia upotevu wa fedha za serikali.
“Kasoro zilizojitokeza zimefanyiwa kazi na mabadiliko ya ukusanyaji wa fedha katika vyanzo vya mapato ndani ya jeshi hilo, vimeimarika ambapo kwa sasa imekusanya shilingi bilioni 12 kutoka bilioni nane,” aliongeza Masoud.
Sambamba na hilo, alieleza kwamba mikakati iliyopo hivi sasa ni kuifanyia marekebisho ya sheria iliyoanzisha jeshi hilo ili kukipa nguvu zaidi kikosi hicho liweze kujiendesha wenyewe.
Kuhusiana na suali la usafi wa miji na maeneo na malipo yanayotozwa na kampuni Green Waste, alieleza kuwa suala hilo lipo nje na kanuni hata hivyo aliahidi kufanyiwa uchunguzi suala hilo na itapobainika sheria itachukua nafasi yake.
Akizungumzia kuhusu ukusanyaji wa mapato katika serikali za mitaa, alisema kumekuwa na mfumo maalumu uliounganishwa na teknolojia ya habari na mawasiliano jambo linalotarajiwa kuleta matokeo chanya na ongezeko la mapato.
Akizungumzia mikopo kwa makundi maalumu alisema, changamoto iliyopo ni kutokuwepo kwa muongozo wa mgawanyo wa fedha hizo kwa mujibu wa sheria namba 7 serikali za mitaa.
Baada ya majadiliano na majibu ya hoja mbali mbali za wajumbe, wajumbe hao walipitisha bajeti kuu ya serikla pamoja na sheria ya matumizi ya fedha na sheria za kodi kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022 utakaoanza julai mosi mwaka huu.