NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto, Nassor Ahmed Mazrui amesema matumizi ya tumbaku na bidhaa zinazotokana na uraibu huo, yamebainika yanachangia ongezeko la maradhi yasiyoambukiza.

Waziri huyo alieleza hayo jana huko katika ukumbi wa wizara ya Afya Mnazimmoja mjini Zanzibar kwenye maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kupinga matumizi ya tumbaku na bidhaa zinazotokana na tumbaku.

Alifahamisha kuwa Zanzibar ina ongezeko kubwa la maradhi yasiyoambukiza kama shindikizo la damu, kisukari, saratani za aina mbalimbali na magonjwa yanayotokana na mfumo wa kupumua, ambapo tumbaku na matumizi ya bidhaa hizo kwa kiasi kikubwa yanachangia.

Alisema inashangaza sana kuona baadhi ya wanajamii wanaendelea sana kutumia tumbaku na bidhaa zake, huku tafiti zikionesha kuwa anayetumia uraibu huo huathirika kiafya hasa kukabiliwa na moja ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

“Umefika wakati jamii iachache na matumizi ya tumbaku na bidhaa zake kwani ni hatari kwa afya. Ukitumia tumbaku ama bidhaa za tumbaku haikuachi salama kiafya dhidi ya maradhi yasiyoambukiza”, alisema.

Alisema pamoja na kwamba Zanzibar ina asilimia saba ya watu wanaotumia tumbaku na bidhaa za tumbaku, hata hivyo kunaongezeko la uingizwaji wa tumbaku na bidhaa zake akitolea mfano wa tumbaku ya kimasai, tumbaku ya India na tumbaku ya Tanga.

Alisema watumiaji wanazisifu tumbaku hizo, lakini wanasahau kuwa kila tumbaku ikiwa kali ndio inaongeza maradhi mwilini kwa haraka zaidi na kubainisha kuwa tumbaku ina sumu zinazoharibu mwili zaidi ya elfu moja.

Kwa upande wake Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya, Dk. Fadhil Abdalla, alisema wataendelea kutoa taaluma kwa jamii ili ifahamu madhara yanayotokana na tumbaku hasa kutokana na kubainika inachangia ongezeko la maradhi yasiyoambukiza.

Dk. Fadhil alisema kuna gharama kubwa za kumgharamia mgonjwa anayekabiliwa na maradhi yasiyoambukiza pamoja na kwamba hakuna dawa za moja kwa moja kutibu maradhi hayo.

Naye Mratibu wa maradhi yasiyoambukiza Zanzibar, Omar Abdalla Ali alisema vita vya kupambana na maradhi vimegeukia kwenye maradhi yasiyoambikiza kuliko ya kuambukiza.

Alisema Zanzibar maradhi ya kuambukiza kama HIV, TB, Malaria yote yapo chini ya asilimia 1, lakini wagonjwa 10 wanaolazwa katika hospitali ya Mnazimmoja sita wanaugua maradhi yasiyoambukiza.

Aidha alisema idadi ya watu wengi wanaolazwa na kufa katika hospitali za Zanzibar ni wale wanaougua ugonjwa wa shindikizo la damu ambapo kati ya wagonjwa 10, sita hufariki.

“Hakuna njia mbadala ili tuepukane na idadi hii ya vifo vinavyotokana na maradhi yasiyoambukiza, lazima tuachane na matumizi ya tumbaku ambayo ni moja ya kichocheo cha magonjwa hayo”, alisema Omar.

Siku ya kuadhimisha udhibiti wa matumizi ya tumbaku hufanyika kila ifikapo Mei 30, ambapo ujumbe wa mwaka huu “jitoe katika matumizi ya tumbaku”.