KHAMISUU ABDALLAH NA MOHAMMED RASHID (DOMECO )

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, imekuwa ikishajihisha vikundi vya mazoezi katika maeneo mbalimbali, ili  kupunguza maradhi yasiyo ya kuambukiza.

Waziri Wa Afya,Ustawi Wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto. Nassor Ahmed Mazrui,  ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mwakilishi wa  Jimbo Kojani Hassan Hamad Omar,  aliyetaka kujua ni lini serikali itaandaa utaratibu wa kuratibu vikundi vya mazoezi vijijini hususa katika maeneo ya Kojani , Chwale na Mchangamdogo.

Alisema mazoezi ya viungo ni moja kati ya njia nzuri za kinga na udhibiti wa maradhi ya kuambukiza, hasa kwa watu ambao shughuli zao za kimaisha zinawafanya kukaa bila ya kuishughulisha miili yao kwa muda mrefu.

Aidha alisema kwa sasa jamii zimekuwa na mwamko na hamasa ya kuunda vikundi mbalimbali vya mazoezi katika maeneo ya mijini na mashamba.

Hata hivyo, alipongeza kwa kusema serikali kwa upande wake imekuwa ikishajihisha uundaji wa vikundi hivyo, katika kila eneo na kuvisajili kupitia taasisi husika  (ZABESA) ikiwemo na wizara inayohusika na michezo na taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali kwa ajili ya kurahisisha utaratibu na usaidizi wa vikundi hivyo.

Aidha alisema kila ifikapo tarehe 1 Januari ya kila mwaka serikali kupitia Idara ya Michezo imekuwa ikiendesha bonanza maalum la vikundi vya mazoezi kutoka Unguja , Pemba na Dar es salaam.

Alisema njia hiyo imekuwa chachu katika kuhamasisha mazoezi ya viungo nchini pamoja na kushajihisha na kuviweka pamoja vikundi hivyo ili kuweza kufikia lengo lililokusudiwa.

Wakati huo huo Naibu Spika wa Baraza Wawakilishi Mgeni Hassan Juma, aliitambisha timu ya Mboriborini  iliyochukua ubingwa wa mashindano  yamle yamle cup mfululizo.

Aidha alisema hivi sasa Mboriborini imebadilika na kutoa vipaji vizuri kwa vijana ikiwemo mchezo wa mpira wa miguu ambao umewapatia ushindi.