Adai anatekeleza nguvu ya Mungu

NA JOSEPH NGILISHO ARUSHAJESHI la Polisi Mkoani Arusha linamshikilia mfanyakazi wa ndani, (jina linahifadhiwa ) akituhumiwa  kumnyonga hadi kufa Mtoto wa mwajiri wake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo, alisema kuwa tukio hilo la kusikitisha limetokea jana majira ya Sasa 12.00 jioni katika mtaa wa olekerian kata ya Olasiti jijini Arusha.

Kamanda Masejo, alisema kuwa Mtoto aliyeuawa ana umri wa mwaka mmoja na nusu na kwamba binti hiyo aliajiriwa kufanya kazi katika nyumba ya Oswald, miezi miwili iliyopita akitokea Mkoani Mara.

Alisema chanzo Cha tukio bado hakijafahamika na mtuhumiwa anashikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi  na upelelezi utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.

Akiongelea tukio hilo mwenyekiti wa mtaa wa Olekerian ,Aminiel Mollel, ameeleza kuwa alipigiwa simu na majirani na baada ya kufika eneo la tukio na kumhoji mtuhumiwa alidai kuwa hilo ni tukio lake la tatu kulifanya kwa kunyonga watoto wa waajiri wake na amekuwa akifanya hivyo kutokana na nguvu za Giza.

“Tulifika na kumkuta mtuhumiwa aliendelea kuosha vyombo bila kujali kuwa ametenda  tukio la mauaji ,tulipo mhoji alisema kuwa hilo ni tukio lake la tatu kufanya mauji ya kunyonga watoto akifanya kazi za ndani maeneo tofauti”alisema Mollel.

Aliongeza kuwa mtuhumia huyo amedai kuhusika na matukio mengine mawili ya kunyonga watoto akiwa mfanyakazi wa ndani maeneo tofauti na amekuwa hakamatwi na polisi kwa sababu anatumia nguvu za Giza .

Mwenyekiti huyo ametoa Rai kwa wananchi wanaotafuta wasichana wa kazi kuacha kuletewa wasichana wasio wafahamu ili kuwasaidia kulea Mtoto .

Mwili wa Mtoto huyo umehifadhiwa katika chumba Cha maiti katika hospital ya Mkoa Mount Meru kwa uchunguzi zaidi .