NA KHAMISUU ABDALLAH

KATIBU Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi, Mhandisi Zena Ahmed Said, amewataka wasimamizi katika taasisi za umma ngazi zote kuwasimamia vyema watumishi waliomo kwenye taasisi zao.

Alisema ni wakati kwa wasimamizi hao kutovumilia vitendo vya ukiukaji wa uadilifu na kutowajibika kwa baadhi ya watumishi jambo linalorejesha nyuma jitihada za serikali katika kuwapatia huduma bora wananchi wake.

Mhandisi Zena alitoa kauli hiyo wakati alipokuwa akitoa maneno ya shukurani kwa niaba ya watumishi wa umma katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma duniani katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil, Kikwajuni.

Alisema ni wajibu wa wasimamizi hao kuhakikisha wanachukua hatua stahiki kwa mtumishi ambaye hawajibiki kwa mujibu wa sheria na kanuni za utumishi wa umma.

“Hata aya za kur-an zimesisitiza kuwawajibisha watu ambao hawafuati taratibu katika kazi zao nasi tusiogope kufanya hivyo kwani usimamizi wa watumishi ni maelekezo ya vitabu vyetu vitakatifu,” alisema.

Aidha alisisitiza kuwa pamoja na kuwa kazi ni ibada lakini ni jukumu la wasimamizi kuwasimamia watumishi wake kwa maelekezo ya Mwenyezi Mungu na kupata fadhila zake.

Alisema, uwajibikaji na uadilifu katika utumishi wa umma ni jambo muhimu hivyo ni lazima kwa watumishi wa umma kuzingatia hilo kwa kila hali.

Aidha alisisitiza kuwa ni jambo jema kwa kila mtumishi katika eneo lake kutoa huduma na kuhakikisha anafanya kazi kwa uadilifu na uwajibikaji mkubwa kwani kutowajibika kwa watumishi kunaweza kuleta madhara makubwa kwa wananchi ikiwemo vifo.

Akizungumzia mfumo wa sema na Rais Mwinyi unaotumiwa na wananchi kutoa malalamiko, Zena alisema mfumo huo umewasaidia wananchi wengi kutatuliwa changamoto zao.

“Hata hivyo wapo baadhi ya wasimamizi wa taasisi mbali mbali ambao wamepewa jukumu la kuangalia mfumo huo kuuchukulia poa na kuona hauna umuhimu,” alisema Mhandisi Zena akiwaonya watendaji hao kuacha tabia hiyo.

Alibainisha kuwa katika kuona serikali ipo makini katika jambo hilo tayari ameshaandika barua kwa wakuu wa taasisi kwa watumishi wawili ambao walizembea kwenye kufanyiakazi masuala yanayopelekwa kwenye taasisi zao ili wakuwachukulia hatua.

“Hii ya kusikiliza changamoto za wananchi na kuzitatua ni kazi kama kazi nyengine yoyote, hatutamvumilia mtu kwa kudharau kero za wananchi zikaachwa kushughulikiwa kwa sababu ya mtu anaesimamia ameamua kuwa mzembe,” alibainisha.

Alisema suala la uzembe linaendelea kutokea maeneo mengi na madhara yake ni makubwa hivyo ni vyema kwa watumishi kuwa makini katika kuwatumikia wananchi.

“Mambo tunayoyafanya mbali na kupata adhabu ya kufukuzwa kazi pia unapata jukumu mbele ya Mwenyezi Mungu hivyo ni wajibu wetu kuwa waadilifu na kutekeleza kazi zetu kama tunavyotakiwa bila ya kumuangalia mtu usoni, unamjua ni jamaa wa kiongozi na kutoa haki kwa wote bila ya kuangalia mambo hayo,” alisisitiza.

Alisema watumishi wa umma wamepewa dhamana kubwa ya kuijenga au kuibomoa nchi yao hivyo ni vyema kwa watendaji kuhakikisha wanawajibika katika majukumu yao na kumtanguliza mungu katika kutenda haki.

Aliwasisitiza viongozi na watumishi kuangalia miongozo inayowaongoza katika kazi zao na kuhakikisha anaifata bila ya kuipindisha.

Aidha Mhandisi Zena alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kuonesha kuwajali watumishi wa umma na wananchi kwa miongozo anayoitoa mara kwa mara, usimamizi wa karibu wa miradi mikubwa ya maendeleo na kupigania haki za kila mtu wakiwemo watumishi.

Hata hivyo alimshukuru kwa kuchukua hatua mbali mbali ambazo zinalenga kuboresha maslahi ya watumishi wa umma na wananchi na kuelekea katika ahadi yake ya kuleta neema kwa Zanzibar.

Aidha alimuahidi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Mwinyi kwamba watumishi wapo tayari kubadilika katika utumishi wao na kuyafanyia kazi yale yote anayoyaagiza ili kuona kila mtumishi anatekeleza wajibu wake katika kutoa huduma bora kwa wananchi.

Mbali na hayo, alimhakikishia Rais Mwinyi kuwa wataendelea kuyafanyia kazi mambo yote wanayoyapata kwa wananchi na hawatoruhusu uzembe kwenye jambo la kushughulikia changamoto za wananchi kwani ni moja ya vipaumbele vyake.