NA ALLY HASSAN, DOMECO

ZANZIBAR ni nchi ambayo michezo hupewa nafasi kubwa kwani watu wengi huweka mapenzi yao makubwa hasa kwenye mchezo wa  soka.

Mbali na soka pia michezo mingine inachezwa kwa kwa kiasi kikubwa sana na imekuwa ikiitangaza vyema Zanzibar kimataifa kwa kufanya vyema kwenye mashindano.

Hali hii inaifanya Zanzibar kuwika na kuonekana zaidi ndani na nje ya Tanzania kwa kutoa vipaji mbali mbali vya wachezaji.

Imekuwa kawaida sasa kuwaona wachezaji wengi wa soka kutoka Zanzibar,wanakwenda kucheza mpira ndani ya Tanzania bara.

Ni ukweli usio fichika ukiachia mpira wa miguu, michezo mingine haipewi kipaumbele na ukizingatia michezo hiyo ndio inayo changia kuitangaza Zanzibar kitaifa na kimataifa.

Mfano ya michezo iliyoipatia sifa Zanzibar tukitoa mpira wa miguu ni mchezo wa Judo, mpira wa Mikono, lakini pia watu  wenye ulemavu wa akili amabo wamediriki kuleta medali za dhahabu hapa nchini.

Ni wazi kuwa ipo haja kubwa ya Serekali kuangalia na kuthamini michezo mengine, ambayo kwa sasa haijapewa kipaumbele ili iweze kuleta tija kwa taifa na kwa jamii kwa ujumla.

Tunaelewa kuwa hali halisi ya nchi yetu ilivyo kiuchumi, kuajiri kila mtu ni jambo lisilo wezekana, ni muda sasa wa kuitupia macho michezo yote ili kuleta fursa kwa vijana walio wengi nchini.

Vijana wengi nchini wanapenda kujishughulisha katika michezo mbali mbali, ila wanakosa watu wa kuwaunga mkono katika kuiendeleza michezo hiyo.

Hivyo ni wakati muafaka sasa kwa serekali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuzidi kuwaunga mkono vijana wote, wanao jishughulisha na michezo kwa kuwatafutia wadau ambao watawanyanyua kitaifa na kimataifa kupitia michezo.

Hivi sasa mpira wa miguu ambao unapewa kipaumbele hapa nchini haupo katika ubora, kutokana na kutofanya vizuri kwa michezo ya ndani na nje.

Mfano mzuri ni nchi ya Marekani mpira wa kikapu ndio mchezo uliopewa kipaumbele kuliko mpira wa miguu, na ndio mchezo unao itangaza zaidi nchi hiyo katika michezo.

Ningependa kutoa ushauri kwa serekali na taasisi zinazo husika katika michezo kuipa kipaumbele michezo yote, ili kutoa fursa kwa vijana na kwajamii kwa ujumla kwani inaonekana inaleta tija kwa taifa.

Vile vile serikali izisimamie kikamilifu taasisi hizo katika kutoa taaluma kwa vijana na kuwahamasisha kushiriki michezo mingine badala ya kuangalia mchezo wa mpira wa miguu pekee.