MWAJUMA JUMA NA KHAIRAT SULEIMAN

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar ya awamu ya nane imeanza kuifanyia kazi migogoro iliyomo ndani ya Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF).

Kaimu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Lela Muhamed Mussa, aliyaeleza hayo katika kikao cha Baraza la Wawakilishi, alipokuwa akijibu suala la mwakilishi wa Mfenesini Machano Othman Said, aliyetaka kujua serikali haioni kwamba muda wa umefika kulivunja shirikisho hilo.

Alisema kwa muda mrefu wameshuhudia migogoro ya shirikisho hilo hata baada ya kufanya uchaguzi na kupekekea kutokwepo kwa rais na makamu wake, jambo ambalo halileti taswira nzuri kwa soka la Zanzibar na kusababisha chombo hicho kufanya maamuzi ya kushangaza ikiwemo kutoa tamko la kutokuwa na  timu zitakazoshuka daraja msimu huu.

Alisema utaratibu wa kufuta klabu au chama cha michezo umeelezwa kwenye sheria namba tano ya mwaka 2010 ya Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar kifungu cha 19 (d) (i-v), ambapo sababu kuu  ni chama kwa makusudi kukiuka katiba na kanuni zake, kujihusisha na siasa za vyama, kufa kwa chama wenyewe au uanzishwaji na uongozi wake uko kinyume na sheria.

Alisema katika kufuatilia migogoro hiyo mwezi huu mrajisi wa vyama vya michezo atasimamia kufanyika kwa mkutano mkuu wa ZFF na uchaguzi wa rais, ili kuimarisha utawala bora ndani ya shirikisho hilo.

Hivyo alisema katika hilo watarajie mabadiliko makubwa ya uendeshaji wa ZFF na imani ya Serikali kwamba, wadau mbali mbali wataunga mkono juhudi hizo za Serikali za kutatua migogoro na kutafuta wadhamini.

Hata hivyo alisema uendeshwaji wa shirikisho hilo unaongozwa na katiba na kanuni yake lakini pia katiba na kanuni za Cecafa, Caf na Fifa.

Akizungumzia kuhusu timu kupanda na kushuka alisema ZFF limeandaa kanuni za mashindano, ambazo ndizo zinazotoa utaratibu wa kupandisha na kushusha kwa kila ngazi ya mashindano, ambapo kabla ya kanuni kufanya kazi zinatakiwa kuidhinishwa na Mrajisi wa Michezo.

“Mheshimiwa Spika sababu zilizopelekea ZFF kutangaza muongozo mpya wa timu kutoshuka daraja ni maamuzi binafsi na hayakuzingatia maslahi mapana ya soka la Zanzibar na ni kwenda kinyume na kanuni za mashindano 2020/2021.

Waziri Lela alisema kamati tendaji ya ZFF ilikaa na kufanya marekebisho ya kanuni zake, kwenye kikao yaliyopendekeza timu kutokushuka daraja kwa msimu huu wa ligi, lakini hata hivyo mapendekezo hayo bado hayajaidhinishwa na Mrajisi wa Michezo na hayawezi kutumika.