MATERA, ITALIA

WAZIRI wa Mambo ya Nje wa Japani, Motegi Toshimitsu anasema nchi hiyo itazisaidia nchi za Afrika kuimarisha miundombinu, wakati ikitilia maanani uwepo unaoongezeka wa China barani humo.

Motegi alielezea dhamira hiyo wakati wa mkutano kazi wa chakula cha mchana na mawaziri wenzake kutoka kundi la nchi 20 zilizostawi zaidi kiuchumi duniani, G20 jijini Matera kusini mwa Italia.

Mawaziri hao walibadilishana maoni juu ya uchumi, jamii na ustawi wa Afrika, kwa kutilia maanani athari iliyosababishwa na janga la virusi vya corona.

Motegi alisema Japani itasaidia juhudi za kujenga mifumo ya afya na tiba barani Afrika itakayojumuisha utoaji chanjo.

Kadhalika alisema Japani itabuni mazingira bora ya ufanyaji biashara kupitia ustawi wa rasilimali watu wanaohusiana na viwanda na uhamishaji wa teknolojia.

Motegi alisisitiza kuwa Japani itasaidia ujenzi wa majengo ya bandarini na miundombinu mingine kwa kuzingatia dhana ya eneo huru na la wazi la Indo-Pasifiki.