Palitokea vita baina ya wenyeji na watanga
Unafahamu kwanini uliitwa msikiti chooko?
NA JUMA RAMADHAN, OUT
MSIKITI Chooko au msikiti wivu ni maneno ya yaliyosimuliwa na ofisa mambo ya kale kisiwani Pemba, Salim Seif Yusuf.
Hapa alikuwa akizungumza na mwandishi wa makala haya juu ya makumbusho ya msikiti huo uliopo Shahia ya Tumbe, wilaya ya Micheweni mkoa wa Kaskazini Pemba.
Msikiti huo ulijengwa katika karne ya 16, mwishoni katika eneo la Chwaka Tumbe, kukiwa na mji ambao ulikuwa ukitawaliwa na Mfalme Haroun ambaye alikuwa ni mtoto wa Sayid Baraghash.
Kabla ya kujengwa kwa msikiti huo, ilikuwa tayari mfalme Haroun alikwisha jenga msikiti mkubwa ambao ulikuwa ukitumika kwa swala ya Ijumaa pamoja na masuala maengine ya kiutawala.
Kama ilivyo kawaida ya viongozi ya kutembelea sehemu mbali mbali duniani, nae mfalme Haroun alifunga safari ya kutembelea mkoa wa Tanga, ambapo katika safari hiyo, alikutana na mwanamke wa Kizigua na hivyo kuamua kumuoa na kumchukua katika mji wake wa Chwaka.
“Kila mke aliwekwa katika nyumba yake, ambapo kuna umbali kidogo kutoka alipo mke mmoja hadi mwengine. Palikuwa na umbali kidogo kutoka mke mdogo na mke mkubwa lakini katika mji huo huo.
Kama kawaida yake, mfalme na wasadizi wake, walikuwa wakiendeleza kazi katika msikiti wa Ijumaa pamoja na kuufanya mikutano mbali mbali, hivyo muda wote alikuwaakiutumia huko ambako ni karibu na nyumba ya mke mkubwa.
Jambo hilo la kukaa mda mrefu huko halikumfurahisha hata kidogo mke mdogo, kwani fikira zake zilimpeleka mbali na kufikiria kama mume wake anakaa kwa mke mkubwa kwa muda mrefu si kwa pirika za msikiti tu.
Hapo mke mdogo akaanza kuingiwa na wivu kadiri siku zikienda mbele, kwa kusema kuwa mume wake hayupo msikitini, bali yupo kwa mke mwenzake, na kwanini hata siku ya zamu yake mume wake anachelewa kurudi nyumbani kwake?
Siku za mke mkubwa mke mdogo hana tatizo, lakini siku ya zamu yake kitendo cha mume wake kuchelewa kurudi na kukaa huko kwa kipindi kirefu, kilimhuzunisha, hivyo alikuwa na wasi wasi mkubwa dhidi ya ndoa yake.
Kutokana na kadhia hiyo, bibi mdogo wa mfalme aliishi bila ya kuwa na furaha kwa kipindi cha muda mrefu ndani ya ndoa yake, baadae aliamua kuomba ruhusa ya kwenda kuwatembelea ndugu na jamaa zake nyumbani kwao Tanga.
Alipofika, mengi aliyafanya yanayohusiana na maisha yake kubwa zaidi ni kusimulia mfumo mzima wamaisha yake kwa wazee wake.
Baada ya wazee kumuelewa vyema mtoto wao walimshauri kumtafutia fundi ili na yeye akajenge msikiti jirani na nyumba yake, Msikiti ambao mume wake ataweza kuutumia pindi akiwa katika maeneo yake, ili kuondosha hofu aliyonayo.