NA JOSEPH DAVID

UONGOZI wa klabu ya Mtibwa umesema harakati za ujenzi wa viwanja viwili vya kisasa huko Manungu zimeanza chini ya usimamizi wa wamiliki wa klabu hiyo ambao ni kampuni ya Mtibwa Sugar.

Akizunguza kwa njia ya simu na mwandishi wa habari hii msemaji wa klabu hiyo Tobias Kifaru, alisema ndani ya wiki mbili zijazo ujenzi wa uwanja wa kwanza, ambao upo Manungu ndani ya mashamba ya miwa utaanza kwani mpaka sasa tofali zinatengenezwa kwa kasi kwa ajili ya kujenga ukuta na majukwaa.

“Si zaidi ya wiki mbili ujenzi unaanza,sasa hivi zinatengenezwa tofali ili tuweke majukwaa uwanja wa zamani. Na upo mkakati mwingine tukimaliza huu tunajenga uwanja mwengine wa kimataifa ambao utakuwa jirani na makazi ya watu” alisema Kifaru.

Aidha, Kifaru aliongeza kuwa kitendo cha bodi ya ligi kuufungia uwanja wao wa Manungu Complex waliokuwa akiutumia hapo awali, kimepelekea kufanya vibaya kwa timu yao kwani wamekuwa wa kikosa faida ya kupata hamasa ya mashabiki wao wanapocheza mechi za nyumbani kutokana na kutumia uwanja wa Jamhuri uliopo mjini Morogoro.

Sababu nyingine zilizowapelekea kuchukua uamuzi wa kujenga viwanja hivyo, ni pamoja na gharama za kulipia hoteli timu ikiwa mjini Morogoro na timu kukosa muda wa kutosha wa kufanya mazoezi.

Aliongeza kuwa hivi wanapambana kuhakikisha wanaibakisha timu yao kwenye ligi kuu chini ya kocha wao Mohamed Badru, ili msimu ujao wapate faida za kucheza kwenye uwanja wa nyumbani, huku wakaazi wa Manungu wakipata fursa ya kuzishuhudia timu za Simba na Yanga zikicheza huko.

Tofauti na misimu mingine ambapo Mtibwa ilikuwa ikitumia uwanja wa Jamhuri kama uwanja wake wa nyumbani kucheza mechi hizo.