ZASPOTI
UONGOZI wa klabu ya soka ya Mtibwa Sugar umesema umejipanga kuhakikisha msimu huu kikosi hicho kinaendelea kubakia katika ligi kuu Tanzania bara (VPL).
Akizungumza na Zanzibar Leo kwa njia ya simu, Kocha Mkuu wa timu hiyo Mohammed Badru Juma, alisema kutokana na mechi kadhaa za mzunguko wa pili walizocheza zimewapa matumaini makubwa ya kubaki katika ligi kuu.

“Matarajio ya kikosi chetu ni kukibakisha ligi kuu kwa kuwashangaza wengi kutoka katika alama ya kushuka mpaka kufikia saba bora,” alisema.
Badru alieleza kwamba alisema mchezo wao wa mwisho waliocheza hivi karibuni waliweza kutoka sare ya goli 1 – 1 na KMC.
Alifahamisha kwamba katika mechi mbili zilizobakia timu yake ina matumaini makubwa ya kufanya vizuri na kuhakikisha inabakia katika ligi kuu.

Alizitaja mechi mbili ambazo wanatarajia kucheza mapema mwezi ujao ni pamoja na JKT Tanzania pamoja na Dodoma jiji ambazo zitakua za mwisho kwa msimu huu.
“Mechi ya juzi tuliocheza na KMC kama tungefunga tungekua tupo mbali lakini hatujakata tamaa matumaini makubwa kufikia malengo tulioyaweka kwa msimu huu.

Sambamba na hayo Badru aliwaomba mashabiki wa klabu hiyo kuendelea kuiunga mkono ili iweze kufanya vizuri na kutimiza malengo wanayojiwekea kila msimu wa ligi.
Mtibwa Sugar yenye maskani yake Turiani Mkoani Morogoro inaendelea kufukuzia kubaki katika ligi kuu Tanzania ambapo hivi sasa ina alama 38 na imebakisha michezo miwili ambayo watacheza na JKT Tanzania na Dodoma jiji.