NA MARYAM HASSAN

VIJANA wawili wenye umri wa miaka 20 kila mmoja akiwemo mwanadada mmoja, wamepelekwa rumande wakituhumiwa kwa kosa la ujambazi.

Chiku Juma Said mkaazi wa Kizimkazi Mkunguni na Ramadhan Khamis Sururu, wamepelekwa rumande na Hakimu wa mahakama ya mkoa Mwera Khamis Ali Simai, baada ya kuwanyima dhamana washitakiwa hao.

Hakimu huyo alisema, kosa waliloshitakiwa nalo halina dhamana, hivyo washitakiwa wote wamerudishwa rumande hadi tarehe iliyopangwa na mahakama.

Mapema, wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Safia Serembe, alidai kuwa washitakiwa hao walitenda kosa hilo Aprili 10 mwaka huu majira ya saa 6:00 za usiku, huko Kizimkazi Mkunguni wilaya ya Kusini mkoa wa Kusini Unguja.

Alidai kuwa, washitakiwa hao waliiba pikipiki moja aina ya ‘roox’ yenye nambari za usajili Z133 LA ikiwa na thamani ya shilingii ya 2,000,000 kwa kukisia, mali ya Makame Haji Makame.

Alidai kuwa, mara na kabla ya kuiba, walimtishia kumchoma kisu tumboni mmliki pikipiki hiyo na kumzuwia safari yake, ili kufanikisha kitendo cha wizi jambo ambalo ni kosa kisheria.

Waliposomewa kosa lao washitakiwa hao walikataa na kuiomba mahakama kuwapa dhamana, ombi ambalo lilikataliwa na upande wa mashitaka.