NA KHAMISUU ABDALLAH
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amewaapisha viongozi mbalimbali aliowateuwa hivi karibuni katika tasisi za serikali.
Walioapishwa ni Asaa Ahmed Rashid ambae ni Mwenyekiti wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Abdulla Mzee Abdulla ambae ni Kamishna wa Kamisheni ya Utumishi wa Umma.
Hafla ya kuapishwa viongozi hao ilifanyika ikulu Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais Othman Masoud Othman, Makamu wa Pili wa Rais Hemed Suleiman Abdalla, Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Injinia Zena Ahmed Said, makamanda wa vikosi vya SMZ na viongozi wengine wa chama na serikali.
Wakizungumza mara ya kiapo hicho viongozi hao waliahidi kufanya kazi kwa uadilifu na ufanisi mkubwa ili kurudisha heshima kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kuonesha imani ya kuwaamini katika kuwatumikia wananchi.
Walisema imani aliyoionesha Dk. Mwinyi kwao ni kubwa na wanadeni la kuhakikisha wanafikia malengo aliyojiwekea katika kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo.
Aidha walisema ni jukumu lao kuhakikisha wanafanya kazi kwa uadilifu na umahiri mkubwa ili kuona serikali inafanikiwa katika malengo yake iliyojiwekea katika miaka mitano ijayo.
“Tunamuahidi hatutamuangusha kwani ametuamini kutupa kazi hii nasi hatuna budi kumuunga mkono katika hilo,” walisema.
Sambamba na hayo waliwaomba watendaji katika tasisi hizo kuwapa ushirikiano katika utelekezaji wa majukumu yao ili lengo lilokusudiwa na rais liweze kufikiwa.