NA JOSEPH NGILISHO, ARUSHA
JESHI la Polisi Mkoani Arusha, linachunguza tuhuma za kughushi mkataba zinazomkabili Nabii, Baraka Ogillo wa kanisa la Christ Synagogue Ministries, ambaye anadaiwa kujaribu kujiuzia eneo la mjane alilokuwa amepangisha lililopo Sakina jijini Arusha, ili hali akijua ni kosa kisheria .
Akiongea na vyombo vya habari mjane Bernadette Changuru alidai amefunga kesi ya kughushi polisi yenye kumbukumbu AR/RB/4121/2021 dhidi ya Nabii Baraka Ogillo.
Alisema Nabii huyo, ambaye ni mpangaji wake kwa madai ameghushi mkataba unaodai ameuziwa eneo na marehemu mumewe lililopo Sakina jijini hapa ,plot namba 32 block FF , baada ya marehemu mumewe, Silasi Chunguru kufariki dunia mwaka 2019.
Alifafanua kwamba Ogillo aliingia mkataba wa upangaji katika eneo hilo na marehemu mumewe miaka 10 iliyopita kwa makubaliano ya malipo ya kila baada ya miezi mitatu.
Alisema Nabii alikuwa akilipa Kodi katika akaunti ya benki ya Azania kiasi Cha shilingi 1,200,000 kila baada ya miezi mitatu, ikiwa ni wastani wa shilingi 400,000 kila mwezi, na mara ya mwisho alilipa Kodi ya miezi mitatu tarehe 20 mwezi wa tatu mwaka huu ambayo Kodi yake imeishia tangu mwezi wa tano mwaka huu.
Mjane huyo anadai kwamba ilipofika Machi 30, mwaka huu ,Nabii Odilo, alimpatia barua inayomtaarifu msimamizi wa mirathi ya marehemu (Bernadette) kwamba April 24, mwaka 2018, kabla ya kufariki aliingia makubaliano ya kuuziwa eneo hilo na marehemu.
Alidai kuwa barua ilieleza kuwa alimpatia marehemu kiasi Cha sh, milioni 24 Kama sehemu ya malipo waliyokubaliana ya shilingi milioni 42 na kiasi kilichobaki cha sh, milioni 18 angelipa kidogo kidogo kwa mfumo wa malipo ya Kodi yaliyokuwa akilipa, Jambo ambalo mjane amedai si kweli kwani marehemu alikuwa akimshirikisha kila Jambo .
“Baada ya barua hiyo nilichukua uamuzi wa kwenda kwa mtendaji wa kata kuripoti juu ya taarifa hiyo ,ambapo Nabii aliitwa ila hakutokea ndipo nilipoamua kwenda polisi kutoa taarifa ya kutaka kutapeliwa eneo na mpangaji wangu”alisema.