BRAZAVILLE, CONGO

VIONGOZI wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Katikati mwa Afrika wamekutana huko Brazaville mji mkuu wa Congo kufuatia kuongezeka hali ya wasiwasi katika nchi ya Chad. Viongozi wa Congo, Angola, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wameshiriki kikao hicho.

Moussa Faki Mahamat Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amesema katika mkutano huo kuwa kipindi cha mpito nchini Chad kinahitaji kuungwa mkono na pande zote. Alisema nchi hiyo itafanikiwa kwa haraka kwa fikra makini, uoni wa busara na ubunifu wa wasomi na wanasiasa wa Chad.

Wakati huo huo Jean Claude Gakosso Waziri wa Mambo ya Nje wa Kongo alizitolea wito pande husika za kisiasa nchini Chad kuzingatia kwanza maslahi ya taifa na kushirikiana kwa uaminifu ili kutimiza yale yaliyokusudiwa katika uongizi wa mpito wa miezi 18 nchini humo.

Chad imekuwa na serikali ya mpito baada ya kuaga dunia mtawala wa muda mrefu wa nchi hiyo, Idriss Deby Itno ambaye aliuawa mwezi Aprili mwaka huu.

Siku moja baada ya kifo cha Idriss Deby, mwanawe wa kiume, Mahamat Idriss Deby alichukua hatamu za uongozi wa mpito na kuahidi kuitisha uchaguzi katika kipindi cha miezi 18. Hata hivyo hali ya usalama nchini Chad inatia wasiwasi huku mivutano ya kisiasa ikiendelea na hivyo kuibua wasiwasi wa kuibuka machafuko zaidi.