INGAWA binadamu anadhurika kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya tabianchi, hata hivyo serikali hazihaweka mifumo ya kutosha kulinda afya za wananchi, hiyo ni kwa mujibu wa shirika la afya ulimwenguni (WHO).

Shirika hilo linaeleza kuwa mabadiliko ya tabianchi yamekuwa mwiba kwa afya ya binadamu kutokana na kusababisha ongezeko la joto, vimbunga na tsunami lakini tathmini imeonesha kuwa ni nchi 1 tu kati ya 5 ndio ina mkakati wa afya kusaidia wananchi kukabiliana na hali hizo.

Tathmini hiyo inaonesha kuwa watu wanafariki dunia kutokana na joto la kupindukia na pia majanga kama vile mafuriko na vimbunga. Halikadhalika masuala ya uhakika wa chakula na upatikanaji wa maji, sambamba na magonjwa kama vile kipindupindu, dengue na malaria.

Mkurugenzi mkuu wa WHO, Dk. Tedros Ghebreyesus anasema kuwa, “mabadiliko ya tabianchi hivi sasa siyo yanasababisha gharama zitakazolipwa na vizazi vijavyo, bali pia ni gharama ambazo watu wanalipa hivi sasa kutokana na afya zao”.

Amesema ni kwa mantiki hiyo basi nchi lazima zitenge rasilimali zinazohitaji dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kulinda afya hivi sasa na za vizazi vijavyo.

Licha ya matokeo ya tathmini hiyo, asilimia takribani 60 ya mataifa husika yamesema kuna hatua kidogo sana au hakuna kabisa katika kutenga rasilimali watu au fedha kwa ajili ya kuchukua hatua za kulinda afya za watu.

WHO inasema kuwa kuweka ajenda ya afya katika michakato ya kitaifa na kimataifa inayohusiana na mabadiliko ya tabianchi kunaweza kusaidia kuelekeza fedha zinazohitajika.

Ripoti hiyo imeonesha kuwa theluthi mbili ya michango ya kitaifa iliyotangazwa katika kukabili mabadiliko ya tabianchi kwa mujibu wa mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi imetaja afya kama sehemu ya hatua za kukabili mabadiliko hayo lakini hakuna hatua za dhahiri katika utekelezaji.

Tafiti za awali za WHO zimebaini kuwa kupunguza utoaji wa hewa chafuzi kwa mujibu wa mkataba wa Paris kunaweza kuokoa maisha ya mamilioni ya watu kila mwaka duniani kote ifikapo mwaka 2050.

Hata hivyo, WHO inasema kuwa mataifa mengi hayana uwezo wa kutumia fursa hiyo kama ilivyopendekezwa, takwimu zikionesha kuwa ni nchi 1 kati ya 44 inaweza kuonesha ushirikiano kati ya sekta ya afya na sekta muhimu zinazochochea mabadiliko ya tabianchi na uchafuzi wa hewa kama vile sekta ya usafirishaji, uzalishaji umeme na nishati itumikayo majumbani.

Kwa upande mwingine, mataifa husika kwenye tathmini yalidhihirisha ushirikiano zaidi kati ya sekta ya afya na sera za mabadiliko ya tabianchi ambapo wamesema ushirikiano huo upo kwenye masuala ya maji, huduma za maji safi na maji taka.