NA FATUMA KITIMA, DAR ES SALAAM

SERIKALI ipo tayari kupokea maoni ya wadau ili kuweza kufanya mabadiliko ya mitaala ambayo kila mtanzania ataruhusiwa kutoa mawazo yake, ili kumuweka vizuri kielimu mtoto wa kitanzania kuajiriwa na kujiajiri.

Hayo yalisemwa  jana jijini Dar es Salaam kwenye mkutano wa kupokea maoni ya wadau kuhusu uboreshaji wa elimu ya awali, msingi na sekondari .

Akizungumza  Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako,  alisema maoni hayo yatatumiwa na Taasisi ya Elimu Tanzania, katika kuimarisha mitaala ya ngazi ya elimu ya msingi ili kuona inatoa ujuzi, maarifa  na kuweka  misingi madhubuti katika elimu.

Prof. Ndalichako alisema mkutano huo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ya kufanya mapitio ya mitaala ya elimu, lengo likiwa ni kujikita zaidi kwenye ujuzi, stadi za kazi na mweleko chanya kwa watoto.

“Naweaomba wadau wa elimu kushiriki kikamilifu ili kuweza kutoa maoni yatakayosaidia Taifa kuwa na mitaala bora kwakuzingatia ujuzi, ambao Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa kielezea na ujuzi ambao wadau mmekuwa na kiu “alisema

Alieleza Serikali imekuwa ikifanya mabadiliko ya mitaala kwa kuangalia mahitaji muhimu kwa Nchi, Kanda, au Dunia, ikiwa ni chachu ya kufanya iendane na hali halisi ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na teknolojia.

Nae, Mwenyekiti wa Baraza la Elimu Tanzania (TET) Prof. Bernadeta Killian, amesema ameagiza uongozi kukusanya maoni, ili kuweza kupata mitaala yenye ubora, na Chuo kikuu cha Dar es Salaam, tayari kimeanza kufanya mapitio ya mitaala yao na kuahidi kuongeza wigo juu ya ukusanyaji wa maoni kwa wadau.

Tangu kupata uhuru mitaala imekuwa ikifanyiwa mabadiliko makubwa mara tano ambapo ilianza na mwaka 1967, ambayo ililenga kuondokana na mitaala ya kibaguzi iliyokuwa ikitolewa na wakoloni.