NA HANIFA SALIM

WAKAAZI wa visiwa vya Njau na Kokota wilaya ya Wete wamelishukuru Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) kwa kutoa punguzo la gharama ya uungaji wa umeme kutoka shilingi 200,000 hadi  shilingi 50,000.

Walieleza hayo kwa nyakati tofauti baada ya kupokea taarifa ya kukamilika ufungaji wa vifaa vya umeme wa jua kutoka ZECO katika visiwa vya Kokota na
Njau.
Ali Issa Khamis ambae ni miongoni mwa wakaazi wa kisiwa cha Njau, alisema, itakapokamilika huduma hiyo itawasaidia katika shughuli zao za kijamii, ikiwemo kuhifadhi samaki wao wakati wanapochelewa kurudi katika shughuli zao za uvuvi.

“Tulikuwa tunauza samaki wetu hata kwa bei ya chini kwa sababu hatuna pa kuhifadhi jambo ambalo lilikuwa linaturejesha nyuma kimaendeleo,” alisema.

Kaimu Mwalimu Mkuu wa skuli ya Njau, Omar Ali Omar alisema, ni vyema wananchi wakatumia fursa hiyo ili kuleta mabadiliko ya maendeleo katika kisiwa chao, kwani huduma hiyo walikuwa  wakiitafuta muda mrefu.

“Tunashukuru katika kisiwa cha Njau kuona tutafikiwa na huduma ya umeme hivi karibuni, kwani sisi walimu tulikuwa tukisubiri kwa hamu kubwa, tunajua itatusaidia kuendesha masomo ya usiku na kambi za masomo kwa wanafunzi wetu,” alisema.

Nae Adam Khamis Khamis mkaazi Kokota, alisema itakapofika huduma hiyo kisiwani kwao itapanua zaidi ukuaji wa biashara zao ambazo zitapelekea kuimarisha uchumi wao.

Ofisa mipango na utafiti wa ZECO tawi la Pemba, Ali Faki Ali, alisema, lengo la kukutana na wananchi hao ni kutoa taaluma kuhusiana na ujenzi wa umeme wa jua pamoja na kuwataka waandae mifumo ya ndani ya nyumba zao.

“Tumekuja kuwashauri muanze kufanya ‘fitting’ katika nyumba zenu, kwa sasa tayari ameshapatikana mkandarasi wa ujenzi wa mitambo na tunatarajia
ifikapo Julai mwaka huu ujenzi huu utaanza,” alisema.
Aidha aliwataka wananchi kutafuta wataalamu ambao wataweza kufanya mifumo (fittingi) ya uhakika katika nyumba zao, ili kuepuka hitilafu ambazo zinaweza kuleta hasara kwao.

Ofisa idara ya biashara wa shirika hilo Pemba, Khamis Ali Abdalla, alisema kwa vile serikali imeamua kuwapelekea huduma hiyo, wananchi wawe tayari na kuthamini juhudi hizo kwa kuleta ushirikiano, ili kufikia malengo yao.
“Tujiweke tayari kuanza kujisajili ili zoezi liendeshwe bila usumbufu,” alisema.

Ofisa uhusiano wa shirika hilo Pemba, Amour Salim
Masoud, alisema harakati za kupeleka umeme visiwani ni gharama kubwa lakini serikali inafanya bidii ili kuhakikisha wananchi wote wanafaidika na huduma hiyo.