NA MWANDISHI WETU
BENKI ya NMB itaendelea kushirikiana serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika mambo mbali mbali, ikiwemo michezo na utalii.
Kauli hiyo imetolewa na Meneja Msimamizi wa Biashara za NMB kwa Matawi ya Zanzibar Abdalla Duchi, wakati akizungumza katika hafla ya kuzindua mashindano ya Zanzibar International Marathon, huko Hoteli ya Park Hayat.
Alisema benki hiyo imeamua kushiriki kudhamini mashindano hayo kwa lengo la kukuza utalii na uchumi wa buluu kwa kuibua vipaji vya vijana .
Alisema wameona ni busara kushiriki na kutoa chachu ya maendeleo ya michezo, kwani benki hiyo ni sehemu ya jamii, ili kuona maendeleo ya nchi hii yanachangiwa na kampuni.
Alisema ya sera ya NMB inaunga mkono vijana hivyo wameamua kushiriki mashindano hayo, kwani wanafahamu kuwa wataibua vipaji vya vijana na baadaye kupata ajira kupitia michezo.
Aidha alisema suala la utalii kwa Zanzibar ni sehemu kubwa nyingine ambayo wanaipa kipaumbele, kwani wamekuwa na ushirikiano mkubwa na ZATO, na hivi karibuni watazindua kadi ili utalii ufanywe kidijitali.
Aliongeza kuwa wataendelea kushirikiana na waendeshaji wa utalii au watu wengine pamoja na vyama vya michezo na wadau wa michezo, ili kuhakikisha Zanzibar inapiga hatua kubwa katika maendeleao ya michezo.
Mapema akuzindua mashindano hayo Kaimu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Lela Mohammed Mussa, alisema mpango wa kufufua mashindano ya mbio za Marathon Zanzibar unalenga kutangaza vivutio vilivyomo ili kuongeza idadi ya wageni nchini.
Alisema mashindano kama hayo yaliwahi kufanyika Zanzibar na kuifanya Zanzibar kutambulika kimataifa, hivyo kuanzishwa tena kwa sasa kunahitaji mikakati imara ili kuwa endelevu.