NAIROBI, KENYA

HUKU joto la kisiasa kilipanda nchini Kenya ambapo uchaguzi mkuu unatarajia kufanyika mwakani, aliyekuwa seneta wa Machakos, Johnstone Muthama amesema ana imani kwamba naibu rais wa sasa William Ruto aana nafasi kubwa ya kuingia ikulu.

Muthama alitoa matamshi haya baada ya kuwepo madai kwamba rais Uhuru Kenyatta na kinara wa chama cha ODM, Raila Odinga wanapanga kuifanyia mabadiliko katiba kupitia mpango wa BBI ili wamzuie Ruto kuwa rais.

Seneta huyo wa zamani alisema Ruto ana nafasi kubwa ya kuwa rais mpya wa Kenya baada ya uchaguzi mkuu wa mwakani pamoja na kwamba anakabiliwa na vikwazo kadhaa.

“Kuwepo au kukosekana Uhuru Kenyatta na mpango wa BBI, lazima naibu rais William Samoei Ruto atashinda kiti cha urais katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka wa 2022”, alisema Muthama.

Wanasiasa wanaomuunga mkono Ruto nchini Kenya wanalalamika kwamba kuna njama kutoka kwa rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga ya kumpinga kuwa rais wa tano wa jamhuri ya Kenya.

Baadhi ya njama za Uhuru na Raila za kutatiza safari Ruto kuingia ikulu ni kutaka kubadilisha katiba, kuunganisha chama cha ODM na Jubilee na kuzuia kampeni za Ruto katika eneo la Bonde la Ufa.

Ruto anajaribu kuiepuka mitego inayoekwa dhidi yake na imedhihirisha wazi kwamba kwa sasa ana mashabiki wengi kulingana na jinsi alivyolakiwa mkoani Nyanza na kaunti ya Nakuru.

Kigogo huyo anaazimia kuwania kiti cha urais kwa tiketi ya chama cha UDA ambacho kilizunduliwa hivi majuzi baada tofauti za kisiasa kushuhudiwa ndani ya chama tawala cha Jubilee.