Ataka watoa huduma kuzingatia vipaumbele

NA ABOUD MAHMOUD

IMEELEZWA kuwa sheria ya msaada wa kisheria nambari 13 ya mwaka 2018 na kanuni zake za mwaka 2019 ni mkombozi kwa watu wasiokuwa na uwezo wakiwemo wanawake na watoto.

Hayo yameelezwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, katika kilelele cha maadhimisho ya pili ya wiki ya msaada wa kisheria Zanzibar katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil, Kikwajuni.

Alisema kwamba kanuni ya 15 ya imeweka wazi kuwa watoa huduma za msaada wa kisheria wametakiwa kuzingatia vipaumbele vya watoto, wazee, mayatima, watu wenye ulemavu na watu wenye kuishi na virusi vya ukimwi, mambo yanayohusiana na migogoro ya ardhi, urithi na mengineyo katika utoaji wa huduma zao.

Hivyo alisema kufanya kazi kwa kanuni hiyo ni moja ya kiashiria kikuu cha kupatikana kwa haki katika jamii.

Alisema katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 imeweka ulinzi tosha wa haki za binadamu, hivyo watoa huduma za msaada wa kisheria wana jukumu kubwa la kuhakikisha wanazilinda haki hizo.

“Katika hili la haki za binadamu nimefarijika kuona kuwa moja katika tunzo zilizotolewa leo ni tunzo maalum ya haki  za binadamu,kwa hili Idara hongereni sana,” alisema.

Sambamba na hayo Othman alisema kuanzishwa na kuendelezwa mfumo rasmi wa msaada wa kisheria hapa Zanzibar ni sehemu ua juhudi za huko Serikali kutambua nchi hii ni sehemu ya dunia.

Hivyo inahitaji kuweka mifumo inayoendana na maendeleo ya kidunia katika fani na nyanja zote.

Aidha alisema kauli mbiu ya mwaka huu ambayo ni “msaada wa kisheria ni chachu ya kumuwezesha mwanamke kiuchumi”.

Alieleza kwamba ni ukweli uliodhahiri na muhimu sana katika jamii kwa kuzingatia kuwa wanawake wanakabiliwa na changamoto nyingi zinazopelekea kutofikia vizuri lengo lao la kujikomboa kiuchumi.

“Nawapongeza sana Wizara na watendaji wake kwa kuendelea na kazi nzuri ya kusimamia na kuratibu masuala ya msaada wa kisheria ikizingatiwa kwamba ni mwaka mmoja na miezi kumi tangu idara ianzishwe lakini mambo yaliofanyika na yanayoendelea kufanywa ni makubwa,” alisema.

Masoud alieleza kwamba pamoja na kazi nzuri ambayo wanaendelea kuitekeleza katika suala la msaada wa kisheria bado wana jukumu kubwa la kuhakikisha wanawasimamia vizuri watoa huduma ili kutoa huduma kwa mujibu wa sheria na viwango vilovyowekwa.

Hivyo aliomba kuzishajiisha taasisi za ndani na za nje kuzisaaidia taasisi za watoa huduma za msaada wa kisheria katika kuwajengea uwezo wa kazi zao hususan katika masuala yanayohusu haki za jamii.

Nae Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Seif Shaaban Mwinyi, alisema ofisi yake imekua mstari wa mbele kuhakikisha inashirikiana na Ofisi ya msaada wa kisheria na shirika na LSF kwa katika kukamilisha malengo yaliyokusudiwa.

Aidha Katibu huyo aliwapongeza wananchi kwa kukubali kutoa mashirikiano na kupata msaada wa kisheria kwa ajili ya kutatua changamoto zinazowakabili.

Nae Mkurugenzi wa Ofisi ya msaada wa kisheria Zanzibar, Hanifa Ramadhan Said, alisema Idara yake imejipanga kisajili wasaidizi wa kisheria wengi zaidi ili wakuwepo katika kila shehia.

Aidha aliwapongeza watoa msaada wa kisheria kwa juhudi wanazozichukua za kuwafikia wananchi wa maeneo mbali mbali kwa ajili ya kuwaletea maendeleo.

Nae Meneja Mkuu wa Shirika la msaada wa kisheria nchini Tanzania (LSF),  Deogratias Bwire, alisema kwa miaka 10 sasa shirika hilo limekua likitekeleza upatikanaji wa haki nchini kwa kutoa ruzuku kwa taasisi zinazosaidia upatikanaji wa msaada wa kisheria.

Hivyo alisema LSF wataendelea kuiunga mkono Ofisi ya msaada wa kisheria Zanzibar katika kuleta maendeleo ya msaada wa kisheria.

Katika maadhimisho hayo taasisi mbali mbali za watoa huduma za msaada wa kisheria na vyombo vya habari vilitunukiwa tuzo ambapo Shirika la magazeti ya Serikali linalochapisha gazeti la Zanzibar Leo lilipata tunzo ya kuwa gazeti bora linaloandika sana habari za Ofisi ya msaada wa kisheria.