NA TALIB USSI, PEMBA

MJUMBE wa kamati kuu ya Chama cha ACT- Wazalendo ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman amesema uzalendo na mashirikiano kwa wananchi wote wa Zanzibar ndio njia pekee ya kumuenzi Maalim Seif Sharif Hamad.

Othman alieleza hayo jana huko katika ukumbi wa chama hicho uliopo Mtambile wilaya ya Mkoani Kisiwani Pemba, akiwa kwenye ziara ya chama ya kutambulishwa kwa viongozi wa mikoa, wilaya na majimbo kisiwani Pemba.

Alisema katika uhai wake Maalim Seif aliyekuwa kiongozi wa chama hicho na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alihimiza ushirikiano miongoni mwa wananchi katika kuijenga Zanzibar.

Makamu huyo alisema kama kuna jambo zuri zaidi la kumuenzi Maalim Seif basi ni kuhakikisha yanatekelezwa yale aliyokuwa akiyasisitiza ikiwemo umoja na mashirikiano miongoni mwa wananchi wa Zanzibar.

“Na sisi wanachama na viongozi kwa pamoja lazima tuyaendeleze yote aliyotuachia mzee wetu, kwani kufanya hivyo ndio tumemuezi kwa vitendo”, alieleza Othman.

Makamu huyo wa Kwanza pia aliwaambia wafuasi wa chama hicho kuwa chama chao kimekuwa nguzo muhimu katika siasa za Tanzania kwa sababu waliwekewa misingi ya umoja, upendo na ukweli miongoni mwa wanachama.

Awali mjumbe wa Baraza kuu la chama hicho Ismail Jussa Ladhu alisema kama wanachama wa chama hicho na wananchi kwa ujumla watakwenda kinyume na kuyasahau yale aliyoyaacha Maalim Seif itakuwa wamefanya kosa kubwa.

“Maalim alipenda sana umoja, upendo kwani aliamini ndio njia pekee Zanzibar kuwa na wepesi katika kuwapatia maendeleo wananchi wake”, alieleza Jussa.

Aliwataka wananchi hao wasikubali kugaiwa baina ya watu wa visiwa vya Unguja na Pemba kwani watu hao kihistoria ni wamoja.

“Asitokee mtu akatugawa baina yetu kwani Maalim mpaka anafika mwisho wa uhai wake katika ulimwengu huu alikuwa anatuhimiza kuwa wamoja”, alisema Jussa.

Maalim akikaribia mwisho wa maisha yake, alihimiza mashirikiano miongoni mwa wananchi hatua ambayo iliasisi kuundwa kwa serikali ya Umoja wa kitaifa ambayo matunda yake yanaonekana katika jamii.

Wananchi wengi kisiwani Pemba wanamuelezea Othman kama Maalim Seif mpya katika medani kisiasa za Tanzania na Afrika kwa ujumla. Chama cha ACT wazalendo kimekamilisha ziara yake ya kumtambulisha kiongozi wao huyo kwa viongozi wa mikoa, majimbo na Matawi kwa upande wa Zanzibar.