NA MADINA ISSA
BENKI ya watu wa Zanzibar wametoa vifaa mbalimbali vya michezo kwa kamati ya maandalizi ya michezo ya Majeshi kwa lengo la kuunga mkono michezo nchini.
Hafla hiyo ya makabidhiano hayo, yalifanyika katika Ofisi ya Benki wa PBZ Mpirani ambapo iliwashirikisha wanakamati wa maandalizi na baadhi ya watendaji wa PBZ.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi vifaa hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya watu wa Zanzibar (PBZ), Dk. Muhsin Salim Masoud, alisema, PBZ imekuwa ikithamini sekta ya michezo na kuahidi kuendelea kuthamini hasa katika udhamini mbalimbali katika sekta hiyo.
Alisema michezo inapelekea kujenga afya na kuwafanya watu kuendeleza umoja jambo hilo ni zuri katika maendeleo ya jamii, hivyo aliwaahidi wanakamati hao kuendelea kudhamini michezo na mengine kwa miaka ijayo.
Aidha aliwataka wapiganaji nchini kuendelea kuwaunga mkono katika taasisi yao ya PBZ, kwa kufanya kazi pamoja na kutoa maoni kwa lengo la kuimarisha benki hiyo ambapo imani yao huduma za kifedha ni moja wapo ya maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Sambamba na hayo, alisema PBZ itaendelea kuimarisha huduma zao za kibenki kwa kuengeza matawi mbalimbali Tanzania bara ambapo hivi karibuni wameweza kufungua matawi ya benki hiyo.
Mapema, Mwenyekiti wa Kamati Kanali Danmian Mtao Majare, alisema, benki hiyo sio mara ya kwanza kudhamini michezo ingawa kwa Kamati hiyo ni mara ya kwanza ambapo aliupongeza uongozi wa PBZ na kuwaomba kuendelea na muendelezo wao huo.
Nae, Katibu wa Kamati hiyo, Kanali Martin Msumari, aliishukuru benki hiyo kwa kufadhili michezo ya baraza la mchezo la majeshi Tanzania, (BAMATA), kwani itainua zaidi sekta ya michezo ambayo imekuwa ikiwaunganisha kwa ukaribu zaidi, kwani michezo ni afya, inaongeza urafiki na ajira.