NA MADINA ISSA

JESHI la Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, limefanya operesheni maalum ya kuwasaka wananchi wanaokiuka utaratibu wa kutokata vyeti vya kusafirishia mazao yao kutoka mashambani kuelekea mjini.

Kamanda wa polisi mkoa huo, Suleiman Hassan Suleiman, aliyasema hayo, makao makuu ya mkoa huo Tunguu wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.

Alisema hatua hiyo imekuja kufuatia kuongezeka kwa malalamiko ya wananchi yanayotokana na wizi wa mazao katika maeneo mbali mbali ya mkoa huo.

Alisema, katika operesheni hiyo jeshi limebaini kuwa wananchi wengi waliokuwa wakisafirisha mazao hawana vibali vya kusafirishia mazao yao kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo ya kutokuwa na uelewa wa kukata vibali hivyo kutoka kwa sheha.

Hivyo, aliziomba taasisi zinazohusika na utoaji wa vibali kutoa elimu kwa wananchi ili kuondosha usumbufu kwa wananchi

Hata hivyo alisema jeshi la polisi mkoani humo litaendelea na operesheni za mara kwa mara na kuwataka wananchi wanaosafirisha mazao kuhakikisha wanakata vibali kwa masheha ili kuepukana na matatizo mbali mbali ya kuzuiliwa mali zao wakati wa kusafirisha na kupata hasara.

Nao wamiliki wa mazao hayo walisema licha ya kuwepo utaratibu wa ukataji wa vibali lakini pia kuna haja ya mamlaka zinazohusika kuangalia upya mfumo wa ulipaji kwani umekuwa ukiwakandamiza hasa ukizingatia wasafarishaji wengi wa mazao hayo ni wakulima na kipato chao ni duni.

Sambamba na hayo walilipongeza Jeshi la polisi kwa uamuzi huo kwani utasaidia kupunguza wimbi wa wizi wa mazao vijijini ambalo limeonekana kushamiri na kurudisha nyuma juhudi zao.