NA ASYA HASSAN
JESHI la Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, limefanya operesheni maalum ya kuwasaka wanaokiuka kukata vyeti vya kusafirishia mazao kutoka mashambani kuelekea mjini.
Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Suleiman Hassan Suleiman, alisema hayo makao makuu ya mkoa huo Tunguu Wilaya ya Kati Unguja, baada kuongezeka malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya wizi wa mazao katika Mkoa huo.
Alisema operesheni hio jeshi limebaini wananchi wengi wanaosafirisha mazao hawana vibali vya Sheha kutoka sehemu moja kwenda nyengine kutokana na kukosa uelewa.
Hata hivyo Kamanda huyo alitumia fursa hiyo kuziomba taasisi zinazo husika na utoaji wa vibali kutoa elimu kwa wananchi, ili kuondosha usumbufu huo.
Hata hivyo, alisema jeshi la Polisi mkoani humo, litaendelea na operesheni za mara kwa mara na kuwataka wananchi wanaosafirisha mazao kuhakikisha wanakata vibali kwa Masheha, ili kuepukana na matatizo mbali mbali ya kuzuiliwa mali zao wakati wa kusafirisha na kupata hasara.
Nao wamiliki wa mazao hayo walisema licha ya kuwepo utaratibu wa ukataji wa vibali, lakini pia kuna haja ya mamlaka zinazohusika kuangalia upya mfumo wa ulipaji kwani umekuwa ukiwakandamiza wananchi hasa ukizingatia wasafarishaji wengi wa mazao hayo ni wakulima wa kipato cha chini.
Aidha wamelipongeza jeshi la polisi kwa uamuzi huo, kwani utasaidia kupunguza wimbi la wizi wa mazao vijijini ambalo limeonekana kushamiri na kurudhisha nyuma juhudi zao.