NA TATU MAKAME

MKUU wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ayoub Mohamed Mahmoud, amewataka wananchi walioekeza fedha zao kwenye kampuni ya Mastalife kuwa wastahamilivu wakati serikali ikiendelea na juhudi za kufuatilia haki zao.

Ayoub alisema hayo Mkokotoni Wilaya ya Kaskazini ‘A’, wakati akizungumza na waathirika walioekeza fedha zao kwenye kampuni hiyo baada ya kamati inayofuatilia haki za wananchi hao kuitisha mkutano wa kusikiliza changamoto zinawakabili watu hao.

Hata hivyo, aliwataka wananchi kuwa na imani na serikali wakati juhudi za kufuatiliwa haki za wananchi zikiendelea kwa  kuomba dua kwani hakuna mtu atakaedhulumiwa kwa fedha ambazo aliwekeza.

Akijibu hoja za wananchi kuhusu kuwapatia vyakula kwa kipindi hiki cha mpito Mkuu huyo, alisema uwezo wa kuwapatia vyakula wananchi haupo ila serikali ya mkoa inaendelea kutafuta mbinu mbadala zitakazowasaidi wananchi kufanya kazi na kupata rizki ili kuendesha maisha yao

“Nduguzangu nisiwafiche uwezo wa kuwapatia vyakula sina ila serikali ya mkoa inaendelea kuchukua jitihada za kutafuta mbinu zitakazowasaidia kufanya shughuli zenu kupunguza tatizo la umaskini kwani tunajua kuwa Wilaya yetu ya Kaskazini ‘A’ ni ya pili kuongoza kwa umaskini kwa wilaya za Zanzibar”, alisema.

Sambamba na hayo, alisema serikali kwa kutumia mamlaka zinaohusika zinaendelea na mchakato wa kutafuta haki za wananchi wote waliowekeza kwenye kampuni hiyo.

Kiongozi wa kamati ya kufuatilia haki za wananchi kupitia kampuni ya Mastalife, Amina Yussuf, aliwataka wananchi kuendelea kumuomba Mwenyezi Mungu kupata haki zao, kwani walioathirika ni wengi ambao waliowekeza kwenye kampuni hiyo.

Mapema wakitoa maoni yao wananchi hao waliiomba serikali kuongeza nguvu kumtafuta mmiliki wa kampuni hiyo, ili kumchukulia hatua pamoja na kuzitafuta haki zao na kuzirejesha kwani wanakabiliwa na wakati mgumu kuendesha familia hasa ukizingatia wengi wao ni maskini.

“Sio kuwa tuliowekeza kuwa tunauwezo wengine tulikopa kwenye vikundi vya uishirika tumefikishwa hadi polisi kudaiwa haki za watu”alisema mmoja wa wananchi hao aliyejitambulisha kwa jina la Fatma Muhamed Juma mkaazi wa Nungwi.

Hata hivyo, waliitaka kamati kufuatilia suala hilo kwa kushirikiana na serikali, ili kuharakisha kupatikana kwa fedha zilizowekezwa kwenye kampuni hiyo.

Itakumbukwa kuwa kampuni ya Mastalife ilifungiwa kufuatia kwenda kinyume na mikataba waliyoandikisha kuendesha biashara ikiwemo kutakatisha fedha, kuandika mikataba ya uongo ya kufanya biashara na mikataba mengine.