TATU MAKAME
SERIKALI imesema juhudi zaidi zinahitajika katika kuondosha dosari mbalimbali zinazobainika katika taasisi za serikali ili kuimarisha nidhamu ya matumizi ya raslimali za umma katika serikali.
Akiwasilisha hotuba ya ripoti ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, utumishi na utawala bora, Haroun Ali Suleiman, alisema kufanya hivyo kutaongeza ufanisi na kutoa matokeo yaliyokusudiwa.
alieleza kwamba Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali ana haki ya kikatiba kutekeleza majukumu yake kwa taasis za umma na kutakiwa kuwasilisha taarifa yake kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambae kupitia Waziri husika taarifa hiyo inatakiwa kuwasilishwa barazani.
Akizungumzia ukaguzi uliofanywa katika mashirika na taasisi zinazojitegemea za serikali ya Mapinduzi Zanzibar, alisema kwa mwaka wa fedha 2019/2020 kuna taasisi zilipata hati chafu, hati zenye mashaka na hati mbaya.
Taasisi nyengine ni Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Wizara ya Afya, Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi na kwa upande wa mashirika ya umma na taasisi zinazojitegemea ni Mamlaka ya Viwanja vya ndege, Shirika la Bandari na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB).
Aidha alieleza kwamba ripoti ya CAG pia inahusisha ripoti ya ukaguzi wa madeni wa Shirika la Meli Zanzibar, ripoti ya ukaguzi kuhusu malipo ya pencheni ya wazee jamii, ripoti ya ukaguzi ukaguzi wa miradi ya kilimo cha pilipili hoho na ripoti ya ukaguzi malipo ya stahiki za walimu.
Alibainisha kwamba ripoti hiyo pia inahusisha ripoti ya ukaguzi wa mfumo wa fedha katika Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, ripoti ya usimamizi na Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), ripoti ya ukaguzi Mfuko wa maendeleo ya jimbo, kitabu cha mifumo ya TEHAMA, ripoti ya kitabu cha ukaguzi maalum kuhusu utekelezaji wa wa maagizo ya Rais wakati alipowaapisha viongozi wakuu.
Akiwasilisha hotuba ya maoni ya kamati ya Baraza la wawakilishi ya Kuchunguza na Kudhibiti Hesabu za serikali (PAC), Mwenyekiti wa kamati hiyo, Juma Ali Khatib, alisema bado udhibiti wa raslimali za serikali ni mdogo hivyo ipo haja ya kuongezwa mikakati ya udhibiti dosari za taasisi hizo.
Alisema zipo taasisi za serikali zinashindwa kuwasilisha taarifa za ukusanyaji wa mapato kwa wakati ikiwemo wakala wa majengo ambayo katika mwaka 2018/2019 na 2019/2020 ilishindwa kuwasilisha taarifa zake za fedha kwa wakati.
Alisema ipo haja kwa viongozi wa serikali kuwa mstari wa mbele katika kuzisimamia sheria, taratibu na utendaji mzima wizara na taasisi zao.
Hata hivyo Mwenyekiti huyo aliwataka watendaji wa ofisi hizo kutekeleza majukumu yao kwa kufuata kikamilifu sheria na taratibu hizo bila ya kushurutishwa.
Akizungumzia changamoto zilizoainishwa katika ripoti hiyo, Khatib alisema ni pamoja na ucheleweshwaji wa kupata majibu ya baadhi ya ripoti za ukaguzi kutoka kwa taasisi zilizokaguliwa na kutojibiwa kwa hoja za ukaguzi kutoka baadhi ya taasisi.
Aliitaja changamoto nyengine ni kucheleweshwa kwa majibu ya ripoti za ukaguzi na kutojibiwa kabisa kwa hoja za ukaguzi jmbo ambalo ni kukosa uwajibikaji na ukiukwaji wa sheria na taratibu za nchi ikiwemo sheria ya ukaguzi namba 11 ya mwaka 2003 pamoja na kanuni, taratibu na miongozo yake.
Nae Mwenyekiti wa Kamati ya Kuchunguza na Kudhibiti hesabu za serikali za mitaa na mashirika (LAAC), Habib Ali Muhamed, aliishauri ofisi ya mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali kufanya ukaguzi katika miradi mikubwa ya maendeleo wakati ikiendelea ili kubaini mapema kasoro kuepusha hasara.
Aidha alisema kamati yake imeshitushwa na taarifa ya kupatiwa hati mbaya Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) na halmashauri ya wilaya ya Kaskazini ‘A’ na kuzitaka taasisi hizo kufanyia kazi hoja zilizotolewa katika ripoti ya CAG.
Wakati huo huo, Haroun alisoma kwa mara ya kwanza mswaada wa sheria ya kuanzisha Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar na kuweka usimamizi mzuri wa shughuli za kiislamu na mambo mengine yanayohusiana na hayo huku Waziri ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Dk. Khalid Mohammed Salum akiwasilisha mswaada wa sheria ya kuanzisha ofisi ya msajili wa hazina na usimamizi wa mali na mambo mengine yanayohusiana nayo kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Jamal Kassim Ali.
Mswada mwengine uliosomwa kwa mara ya kwanza kabla ya baraza hilo kuakhirishwa hadi mwezi Septemba mwaka huu, ni mswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbali mbali na kuweka masharti bora ndani yake uliosomwa na mwanasheria mkuu wa serikali ya mapinduzi Zanzibar, Dk. Mwinyi Talib Haji.