NA MWANDISHI WETU
“NIKUMBATIE mwenye wivu atazame,Nikumbatie roho yake imuume
Nikumbatie mwenye wivu alalame,Nikumbatie akujue wangu mume
Njiani nikipita arudi kinyume nyume,Kata kiu yeye Fanta mi sina habari nae
Ajijue cheo chake mina yeye hatufanani,Atuone ashituke anijue mimi nani
Cheza na mimi mpenzi cheza name kwa helenzi,Mambo mazuri laazizi ndo hayataki haraka”

Ni moja ya beti katika nyimbo maarufu za muziki wa taarab visiwani Zanzibar na Tanzania kwa ujumla wa wimbo unaojulikana kwa jina la ‘Nikumbatie’ ambao ulipigwa katika kundi la East African Melody.
Maneno hayo ni miongoni mwa wimbo mzima ulioghaniwa na mwanadada mwenye sauti ya kumtoa nyoka pangoni si mwengine, ni bibie Rukia Ramadhan Ali.
Rukia ni msanii mahiri katika anga la muziki wa taarab ndani na nje ya Tanzania ambae kila kona ya dunia anajulikana kutokana na kipaji chake alichojaaliwa na muumba wake.

Msanii huyo ambae hapendelei kuitwa malkia wa mipasho kutokana na kutopendelea kuimba nyimbo za kupashana na kuelekeza zaidi nguvu zake katika nyimbo za mahaba na kubembeleza.
Nilipomuuliza anajisikiaje kuitwa jina hilo la malkia wa mipasho,hakuonesha bashasha wala haiba yake ya kawaida ya kutabasamu na akajibu ‘sitaki kuitwa malkia wa mipasho kwa sababu siimbi wala sifikirii kuimba mipasho’.
Jibu hilo lilinifanya nishangae kidogo kwa vile nyimbo za mipasho ndio zaidi hivi sasa zinazowapa umaarufu mkubwa waimbaji wake kiasi cha kumuuliza nini sababu ya msimamo wake huo.

“Mimi ni msanii ninaependa zaidi taarab asilia ambayo lugha ya mashairi yake ni ya kiungwana,haina maneno makali tofauti na taarab ya kisasa,wanaimba tu lakini haina maadili ya Kizanzibari au taarab kwa ujumla,”alisema bila ya kutaka kuingia ndani zaidi.
Nilipotaka kujua alipoanzia hadi alipofikia,Rukia hakukataa tulikwenda hatua kwa hatua hadi mwisho wa mazungumzo yetu,alipoanzia alipofikia na matarajio yake ya baadae.

Msanii huyo alisema alijitosa rasmi katika fani ya muziki mwaka 1974 katika kikundi cha tawi la Afro Shirazi Party la Mwembeshauri chini ya mwalimu wake, marehemu Khamis Shehe.

Alisema wakati huo walikusanywa watoto wengi wa mtaani hapo kwa ajili ya kufundishwa uimbaji na baada ya mafunzo ya muda walipelekwa majaji wenye uelewa mpana wa muziki huo na uimbaji kwa kuwachuja vijana hao.

Rukia alikuwa miongoni mwa vijana waliopenya katika mchujo wa majaji hao na hapo ukawa mwanzo wa mafanikio yake kwa vile kupita huko kulimfanya apelekwe katika klabu maarufu ya taarab visiwani humu ya Culture Musical yenye maskani yake katika mtaa wa Vuga mjini Unguja.

Alianza mazoezi katika klabu hiyo na hatimae kuanza kuimba akiwa bado mwanafunzi wa skuli na hivyo kuweza kubeba majukumu yake yote ya usanii na masomo skulini.
Alisema alianza rasmi kuanza kupanda jukwaani akiwa na kundi lake la Culture na nyimbo yake ya kwanza ilijulikana kwa jina la ‘Kukupenda sana ndilo kosa langu sitofanya tena naapa kwa Mungu,Nilioyaona yanatosha kwangu’.

Kutoka kwake huko kuliwashtua wazazi wake ambao waliona kwamba anajikita zaidi katika uimbaji badala ya kuzingatia masomo yake, hivyo ilimsababishia kuhamishwa Zanzibar na kupelekwa Dar es Salaama kuendelea na masomo.

Msanii huyo mahiri alieleza kwamba alikaa jijini humo kwa muda wa miaka minne na kuendelea na masomo katika skuli ya msingi ya Temeke kabla ya kurejea Unguja kuendelea na masomo yake katika skuli ya Rahaleo, Kidutani ndogo na kubwa ambapo alimalizia kidato cha nne.

Kurejea kwake Unguja kulimfanya arudie tena kwenye muziki wa taarab na kwa bahati mbaya au nzuri hakurejea tena katika kundi lake la awali bali alihamia kwenye kundi mama la Nadi Ikhwan Safaa.

Alisema akiwa ndani ya kundi hilo,lenye maskani yake katika mtaa wa Kokoni mjini Unguja, aliweza kuimba nyimbo kadhaa ambazo zilimjengea jina na kumpa umaarufu zaidi.
Miongoni mwa nyimbo hizo ni pamoja na Nnazama, Nadra na Sadfa,Hidaya, Baada ya dhiki faraja,Niapishe na nyengine nyingi ambazo zote hizo zinaendelea kupendwa hadi hivi sasa.

Rukia, alisema kuanzishwa kwa kundi jipya la taarab la Bwawani ambalo lilikuwa linamilikiwa na hoteli ya Bwawani kulimfanya ahame katika kundi lake hilo chini ya msanii mahiri, marehemu Mwalimu Abdallah .
Alisema kikundi hicho cha Bwawani hakikudumu muda mrefu kwa vile kilivunjika,lakini, kabla ya kuvunjika msanii huyo alifanikiwa kukiimbia kikundi hicho nyimbo kadhaa zikiwemo Nidhibiti,na Nadekea changu.