NA MARYAM HASSAN
Hamadi Mohammed Haji (42) mkaazi wa Kwarara, anayetuhumiwa kutenda makosa matatu ya ubakaji, kutorosha na kulawiti mtoto wa kike wa miaka 15, amepelekwa rumande hadi Juni 16 mwaka huu kesi yake itapoanza kusikilizwa ushahidi.
Mshitakiwa huyo alipewa amri hiyo na Hakimu Zired Abdulkarim, baada ya kuiomba mahakama impatie dhamana, lakini alikosa fursa hiyo kutokana na makosa ya kubaka na kulawiti hayana dhamana.
Hakimu huyo alisema, mahakama yake haina uwezo wa kisheria wa kutoa dhamana dhidi ya makosa hayo na kumuamuru kwenda ruamande.
Mapema, mara baada ya kufikishwa mahakamani hapo, Mwendesha Mashitaka, Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Fatma Saleh, alimsomea makosa yake mshitakiwa huyo ambayo alikataa.
Alidai kwamba, mtuhumiwa huyo alimuingilia kinyume cha maumbile mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 15 (jina linahifadhiwa).
Alidai kwamba, kati ya mwezi Disemba mwaka jana na mwezi Januari mwaka huu kwa siku mbili tofauti, alimuingilia mtoto huyo majira ya saa 12:00 za jioni huko Kwarara wilaya ya Magharibi ‘B’ mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Aidha alidai kuwa, kabla ya kutenda kosa hilo, alimtorosha mtoto huyo kutoka nyumbani kwao na kumpeleka nyumbani kwake bila ya ridhaa ya wazazi wake, jambo ambalo ni kosa kisheria.
Sambamba na makosa hayo, mshitakiwa huyo apia alidaiwa kumbaka mtoto huyo aliye chini ya uangalizi wa wazazi wake, jambo ambalo ni kosa kisheria.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 16 mwaka kwa ajili ya kusikilizwa, kutokana na upelelezi wake tayari umesha kamilika, kwa mujibu wa madai ya upande wa mashitaka.