NA LAYLAT KHALFAN

SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC), limeiomba serikali kuangalia upya kodi ya majengo iliyopendekezwa kuanza kutozwa kwa wananchi katika mwaka ujao wa fedha.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Kikwajuni, kuhusu bajeti ya serikali iliyowasilishwa katika Baraza la Wawakilishi hivi karibuni, Katibu Mkuu wa ZATUC, Khamis Mwinyi Mohammed, alisema ni vyema serikali ikatafuta vyanzo vyengine vya mapato kutokana na hali za wananchi wengi wana hali duni kimaisha.

“Baadhi ya wananchi hadi sasa wanaishi katika nyumba za udongo kutokana na kutokuwa na kipato kidogo, hivyo kutokidhi haja,” alisema mwalimu Khamis.

Aidha aliomba kuimarishwa kwa hali za wananchi wakiwemo wafanyakazi kwa kuwa ndio walipa kodi wakubwa na kuvishirikisha vyama vya wafanyakazi wakati wa uandaaji wa bajeti ili viweze kutetea maslahi ya wafanyakazi na wananchi kwa ujumla.

“Inasikitisha kuona vyama vya wafanyakazi havishirikishwa katika uundaji wa bajeti ili kuwasilisha maoni au mapendekezo yao kabla ya kuwasilishwa barazani,” alisema.

Aliongeza kuwa bajeti imeeleza wazi hali ya uchumi wa nchi umeimarika hivyo ni vyema kuiangalia vyema mishahara ya wafanyakazi ili waweze kumudu hali zao za maisha.

Naye Mwenyekiti wa shirikisho hilo, ALi Mwalimu Rashid, alisema licha ya mfumuko wa bei na kodi na ushuru kupungua, bado bei za bidhaa za vyakula ipo juu, hali inayopaswa kudhibitiwa ili kutoa unafuu wa maisha kwa wananchi hasa wafanyakazi.

“Serikali inajitahidi kupunguza kodi na ushuru kwa bidhaa mbali mbali nchini lakini cha kushangaza wafanyabiashara bado hawapunguzi bei za bidhaa zao,” alisema.

Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Huduma za Umma (ZAPSWU), Mwatum Khamis Othman, alisema wafanyakazi wa Zanzibar wanalipa kodi nyingi ikilinganisha na wa Tanzania bara hivyo ni vyema serikali ikaangalia upya na kuweka mfumo bora wa utozaji kodi hiyo.

Akiwasilisha bajeti kuu ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022, Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais, Fedha na Mipango, Jamal Kassim Ali, aliliambia baraza kwamba katika mwaka huo, serikali inatarajia kuanza kukusanya kodi ya majengo baada ya mfumo kukamilika.

Alieleza kuwa hatua hiyo imelenga kuimarisha mapato katika mwaka huo wa fedha na kupendekeza kutoza kodi ya shilingi 10,000 kwa nyumba ya kawaida na shilingi 10,000 kwa kila ghorofa kwa mwaka.